Sakata
la msichana wa kitanzania, Ummul- Khayr Sadri Abdulla (19), anayedaiwa
kutaka kujiunga na kikundi cha ugaidi cha Al-Shabaab, linazidi kuchukua
sura mpya baada ya madai kuwa alitoroka chuoni Sudan wiki moja kabla
ya kukamatwa nchini Kenya.
Binti
huyo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa Afrika kilichopo Sudan,
aliyekuwa akisomea udaktari mwaka wa tatu, kabla ya kukamatwa Machi 30,
mwaka huu, alikuwa ameshatoroka chuoni hapo tangu Machi 22 na ndugu
zake walikuwa wanamtafuta.
Akizungumza,
babu wa binti huyo, Nassor Said Nofli, alisema kuwa taarifa za kupotea
zilitolewa na dada yake mkubwa, Sumaiyya Sadri Abdulla (20), ambaye pia
anasomea udaktari mwaka wanne katika chuo hicho.
Anasema familia ilishtushwa na taarifa za kupotea kwa mtoto wao baada ya dada yake kumkosa chuoni hapo.
Nofli
alisema ilipofika Machi 23, siku ya Jumatatu hakuonekana darasani wala
hosteli (bweni) huku dada yake akiendelea kumtafuta.
Anaendelea
kusimulia kuwa ilipofika siku ya Jumanne ilitolewa taarifa kwa baba
yake aliyeko Oman kikazi, Dk. Sadri Abdulla Said, pamoja na ndugu
wengine waliopo Pemba, Unguja na Dar es Salaam.
Hata hivyo, baba wa mtoto huyo aliwajulisha kuwa atasafiri Machi 25 kuelekea Sudan ili kusaidia kumtafuta.
Alisema
kuwa tarehe ambayo baba yake alipanga kusafiri, alikosa hati ya
kusafiria na kuahirisha safari hadi alipopata hati ya kusafiri Machi 27.
“Hizi
taarifa za kupotea kwa binti yetu zilitushtua na ilitulazimu kuomba
maombi maalum ya kumuombea “Dua” ili aweze kuonekana na akiwa salama kwa
sababu Sudan kama unavyoielewa ni nchi yenye matatizo ya kivita ,”
alisema.
Nofli
alisema taarifa za kukamatwa kwa mtoto wao wamezisikia kupitia vyombo
vya habari. Alisema wanavishukuru vyombo vya dola kwani familia ilikuwa
inamtafuta na hawakujua alipo.
Alisema kama asingekamatwa inaelekea angejiingiza katika vitendo viovu ambapo familia ingeweza kumkosa binti huyo.
“Kitendo
cha polisi kumkamata imetusaidia na pia wamesaidia kumuokoa yule mtoto
kutokujiingiza kwenye hicho kikundi kwani angeweza kuuliwa ama kupotea
katika kundi hilo,” alisema.
Alieleza kuwa mbali na binti wao kuendelea kushikiliwa na polisi, wanaamini kuwa vyombo vya sheria vitatenda haki.
Nofli
alisema anachokitambua ni kwamba binti huyo alikuwa bado hajajiunga na
kikundi hicho, hivyo familia ina imani haki itatendeka.
“Familia
kwa ujumla tunashukuru kukamatwa kwake kwani ni heri kwake na kwetu kwa
kumuokoa katika tukio hilo tunaamini haki itatendeka,” alisema na
kuongeza:
“Ninavyoona
mimi huyu mjukuu wangu hana kesi ya kujibu kwa kuwa bado hakuingia
katika kundi hilo la ugaidi na ninaamini polisi inamshikilia ili
kuwakamata magaidi wa kweli.”
Kadhalika
alisema jambo lingine lililoishtua familia yake ni pale vyombo vya
habari vilivyoeleza kuwa wazazi wa binti huyo ni wahadhiri wa chuo hicho
ambacho watoto hao wanasoma jambo ambalo si la kweli.
Alisema
jambo hilo limewashtua kwa kuwa linaonekana kuwa wazazi hao wamehusika
katika kumsukuma mtoto wao kutaka kujiingiza katika vikundi hivyo
viovu.
Aidha
akizungumzia madai ya binti huyo kutaka kuolewa na askari mmojawapo wa
kigaidi, alisema ndoa hiyo wasingeitambua kwa kuwa inakwenda kinyume na
sheria za ndoa katika uislamu.
Hata
hivyo, Taarifa za awali zilionyesha kuwa, binti huyo akiwa na wenzake
wawili, Khadija Abubakari Abdulkadir na Maryam Said Aboudall,
walikamatwa katika jimbo la El -Wak mpakani mwa Kenya na Somalia.
Inaelezwa
pia binti huyo alikuwa katika harakati za kuvuka mpaka na kuingia
Somalia kwa lengo la kujiunga na kikundi cha ugaidi na baadaye kuondoka
kutoka Mogadishu kwenda Syria kujiunga na kikundi cha kiislamu
kinachojulikana kama ISIS ambapo angeolewa na wapiganaji wa kikundi
hicho.
Hata
hivyo, taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El –Wak, Nelson
Marwa, zinaonyesha kuwa wasichana hao watatu walikuwa wanakwenda Somalia
kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa
mhanga.
Tulizungumza
na Mhadhiri wa Sheria na Shariah kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha
Morogoro, Tawaqal Hussein, ambaye alisema kwa mujibu wa dini ya kiislamu
hakuna ndoa kama hizo na kwamba wanaofanya hivyo ni kosa kubwa mbele ya
Mungu.
Alisema
sababu ya kutotambulika kwa ndoa hiyo ni moja ya masharti yanayotakiwa
kufanyika ni kuwepo na ridhaa kutoka upande wa wazazi wa kiume kutoka
kwa mtoto huyo wa kike.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Hellen Kijo Bisimba, alisema
kama alikwenda kuolewa haina haja ya kukamatwa kwani suala la ndoa lipo
kijamii.
Lakini
akaongeza kwa kusema kuwa endapo atakuwa anakwenda kujiunga na kikundi
hicho cha ugaidi na uthibitisho ukapatikana ana haki ya kushtakiwa.
"Masuala
ya kuolewa ni ya kijamii na kila mtu ana haki ya kuolewa na mtu yoyote
hata Osama alioa wake wawili, hapo kinachotakiwa ni kuangalia kama huyo
msichana anakwenda kufanya ugaidi au la maana mimi nilisikia kama huyo
msichana anataka kujiunga na hicho kikundi cha kigaidi, lakini kama
anakwenda kuolewa ina maana familia ina taarifa," alisema Bisimba.
Kwa
upande wake, Profesa Abdallah Safari alisema sheria inaruhusu mtu
kuolewa na mtu yeyote na kwamba kuolewa na gaidi sio kosa, hivyo kosa
litajitokeza endapo mtu anakwenda kushirikiana naye katika kufanya
ugaidi.
"Hivi
ni watu wangapi wanaolewa na wezi ama jambazi na hata mafisadi wa
Escrow, uovu wa mtu unabaki pale pale huwezi kumpa mtu mwingine,"
alisema Profesa Safari.
Profesa
Safari alisema kila nchi ina sheria zake za ugaidi na endapo ikibainika
alikwenda kufanya vitendo hivyo atashitakiwa kwa mujibu wa sheria ya
ugaidi ya nchini Kenya.
Aliyekuwa
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, alisema
kimsingi katika masuala ya ndoa hakuna kuchaguliana kuolewa na gaidi au
la.
Alisema ndoa ina masharti yake ambayo yanatakiwa kufuatwa hata kama ni mtuhumiwa una haki ya kufunga ndoa.
"Ndoa
hazivunjwi kwa sababu ya kutiwa hatiani, kosa litajitokeza kama
mwanaume huyo atakwenda kushirikiana katika vitendo vya ugaidi,"
alisema.
Hata
hivyo, mpaka sasa wasichana hao bado hawajafunguliwa mashtaka yoyote
japo mahakama ya nchini humo imeliruhusu jeshi la polisi kuwashikilia
kwa siku 20 kwa ajili ya upelelezi.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )