Featured
Loading...

Kiingereza Kibovu cha Rais Magufuli Chaibua Jipu la Miaka 55


KATI ya mambo mawili yaliyofanywa na Rais John Magufuli wiki iliyopita, moja lilinifurahisha; jingine lilinisikitisha. Nitaanza na lililonifurahisha, anaandika Ansbert
Ngurumo.

Rais Magufuli, akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alitumia Kiswahili kuhutubia marais wenzake na washiriki wengine, katika ukumbi wa hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.

Alinifurahisha jinsi alivyotumia fursa hiyo kusisitiza masuala nyeti ambayo, ama angependa yasimamiwe au yalimkera na aliagiza yasahihishwe.

Rais alisisitiza mambo kadhaa. Kwanza, alizungumzia haja ya nchi wanachama kuvumiliana, kwani kila moja ina matatizo yake.

Pili, alisisitiza umuhimu wa sekretarieti kubana matumizi. Akasema wanatumikia nchi maskini, kwa ajili ya wananchi maskini; hivyo wanapaswa kufanya kazi wakijielekeza kuokoa fedha ili kuelekeza nguvu katika huduma.

Alitoa mfano wa gharama za ukumbi waliotumia kwa ajili ya mkutano huo, katika Hoteli ya Ngurdoto, akisema hesabu zinaonesha kila mshiriki amelipiwa dola 45.
Akasema kama mkutano huo ungefanyikia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Arusha (AICC), kila mjumbe angelipiwa dola 30.

Akatoa mfano kwamba dola 15 ambazo zingeokolewa zingeweza kusaidia ununuzi wa madawati au kuchangia gharama za usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
Mambo haya yatakuwa yamemjengea Rais Magufuli taswira chanya mbele ya wenzake na jamii ya kimataifa.

Hata wananchi wake waweza kuwa walijisikia vizuri kwamba rais wao amethubutu kukumbusha wenzake masuala muhimu waliyopuuza kwa muda mrefu.
Na amefanya hivyo mapema kabisa mwa kipindi cha uenyekiti wake. Ameweka mweleleko mpya unaosisitiza utumishi badala ya utawala.

Hata hivyo, licha ya uzuri wa hoja zake, kuna moja ambalo lilionekana kukera wengi, wakiwamo wasaidizi wake wa karibu.

Nilibahatika kuzungumza na baadhi ya wasaidizi wake. Wengine walisema kwa uwazi; wengine wakakwepa kuzungumza kwa uwazi.

Baadhi ya wasaidizi wa rais, viongozi wa serikali, na wananchi wasomi makini, wameonekana kuchukizwa na jinsi Rais Magufuli alivyotupia maneno ya Kiingereza, hapa na pale katika hotuba yake.
Zipo sababu za mtu kuonekana amechukia. Mambo mazuri niliyozungumzia hapo juu yangeweza kusisitizwa vizuri tu kwa Kiswahili bila kuchomeka Kiingereza.

Au kama mzungumzaji aliamua kuchomeka Kiingereza, basi alipaswa achomeke Kiingereza sanifu.
Yafuatayo ni baadhi ya maneno ya Kiingereza aliyochomeka Rais Magufuli, ambayo hayakupendeza wasikilizaji. Ninaweka hapa mifano mitatu:

“…We are supposed to look each other as one family.”
“Kila siku they come with a special proposals. And that proposals is always positive proposals. Not negative proposals…”
Count on me. I don’t know to whom interest…”
Hotuba ya Rais Magufuli imeibua maneno mengi kutoka kwa watani wake wa kijamii na wa kisiasa.
Nimesikia mmoja akisema, “…sasa naelewa kwanini rais hakuhudhuria hafla ya mabalozi aliyoandaa mwenyewe Ikulu mwezi uliopita.”

Mwingine akisema, “…kumbe ndiyo maana mgombea urais wa UKAWA alipoambiwa mdahalo akasema angeshiriki kama ungeandaliwa kwa Kiingereza.”

Mwingine akidiriki kulinganisha Kiingereza cha Jacob Zuma, Rais wa Afrika Kusini, (ambaye hakukwea madarasa na kutafuna karatasi za vitabu vingi); na kile cha Dk. Magufuli, mwenye shahada ya tatu – ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mzazi mmoja jijini Dar es Salaam amesema Kiingereza cha Magufuli kimesababisha ugomvi kati yake na mtoto wake.

Mzazi huyo hakufurahishwa na kitendo cha mtoto wake cha kuchambua makosa ya kisarufi katika “Kiingereza cha rais.”

Hoja yangu ni ipi? Rais kujua au kutojua Kiingereza? Hapana! CCM ina kigezo cha mgombea urais kuwa angalau na digrii moja. Hicho ndicho walitumia “kumzuia” Augustine Mrema.
Sasa huyu mwenye shahada anatarajiwa walau ajue vema lugha mbili kuu, kikiwemo Kiingereza. Tuangalie hoja zifuatazo:

Kwanza, kwa kuwa rais amejifunza lugha hiyo na atakuwa ameitumia kujifunzia masomo mengine hadi kupata digrii ya uzamivu, anapaswa – siyo tu kuielewa bali hata kuiheshimu – na kuitumia inavyopasa.

Pili, rais hakuwa na sababu ya kutumia maneno ya Kiingereza. Kama alikuwa ameamua kuchanganya Kiswahili na Kiingereza, angetumia Kiingereza sanifu.

Tatu, rais kukosea maneno ya kawaida na kuzungumza Kiingereza “ndivyo-sivyo,” amekuwa mfano mbaya kwa watoto wanaojifunza lugha hiyo, huku wakigombezwa na walimu wao kwa makosa ambayo hata rais anafanya.

Nne, washauri wa rais wamwandalie hotuba. Katika mazingira haya ndipo uzuri wa hotuba zilizoandikwa unapoonekana. Angeweza kusema maneno haya kwa kuyasoma. Yawezekana hata Kiingereza kingenyoshwa, kama angetaka kiwemo.

Tano, kwamba mwalimu wa zamani wa kemia katika shule ya sekondari, ambaye sasa ni msomi wa ngazi ya shahada ya uzamivu katika kemia, anapokosea vitu vidogo lakini muhimu kama hivi, hatoi mfano mzuri kwa watoto wetu ambao wanagombezwa na walimu na wazazi kila wanapokosea Kiingereza kama alivyofanya.

Sita, rais ajenge utamaduni wa kusikiliza washauri wake Ikulu – kama alikuwa hajajenga tabia hiyo. Ni kwa njia hiyo aweza kuepuka makosa ya aina inayojadiliwa. Akubali kusoma hotuba alizoandika au alizoandikiwa na washauri wake.

Saba, ujengwe utaratibu wa kudumu kwa viongozi wetu kuenzi Kiswahili na kukitumia katika mikutano ya kitaifa na kimataifa, ndani na nje ya nchi. Kiswahili kimeshakua. Kama Tanzania tunajiita kitovu cha Kiswahili, tuoneshe kwa vitendo kwamba tunaweza kuipa dunia lugha ya kazi.
Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita, katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika, wakati Benjamin Mkapa akiwa rais, alihutubia viongozi wenzake kwa Kiingereza sanifu.

Ilipofika zamu ya Joachim Chissano, aliyekuwa rais wa Msumbiji, akahutubia kwa Kiswahili mwanzo hadi mwisho. Tulimsema Rais Mkapa kwamba alikuwa amenyang’anywa fursa adhimu ya kumiliki Kiswahili na kuonyesha kuwa Tanzania ndiyo kisima cha Kiswahili.

Tangu mwaka 2005, Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika, kikiwa lugha pekee yenye asili ya bara hili.

Tunatambua kuwa viongozi wetu wengi wanajua Kiswahili kuliko Kiingereza.
Ni vema basi watumie lugha yao kuliko lugha ya kigeni inayowapa shida katika kuwasiliana na wenzao.
Mwaka 2007 nilialikwa kutoa mhadhara katika Kongamano la Highway Africa, lifanyikalo kila mwaka katika Chuo Kikuu cha Rhodes, Grahamstown, Afrika Kusini. Mada yangu ilihusu jinsi ya kublogu kwa Kiswahili.

Katika utafiti wangu, niligundua kuwa Kiswahili kimekua kuliko wengi wetu wanavyofahamu. Niliwaeleza wasikilizaji kutoka nchi zote za Afrika kwamba Kiswahili ni moja ya lugha zinazokua kwa kasi duniani.

Katika Afrika pekee kilikuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 100. Katika Afrika Kusini mwa Sahara, Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kuliko lugha nyingine zote.

Katika maeneo kadhaa ya Afrika, Kiswahili kinatumika Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Malawi, Sudan, Comoro na Malagasy.
Vyuo vikuu zaidi ya 100 duniani vina programu ya kufundisha Kiswahili. Vituo kadhaa vya redio vya nchi mbalimbali duniani vina idhaa ya Kiswahili.

Mifano michache ni BBC, Uingereza; Radio Deutsche Welle, Ujerumani; Nippon Hoso Kyokai (NHK), Japan; Voice of America (VoA), Marekani; Radio China, China; Radio Cairo, Misri; Radio Moscow International, Urusi; Radio Sudan, Sudan; Channel Africa ya Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), Radio France International (RFI), Ufaransa; na Radio India, India.
Nilipokuwa Uingereza, moja ya kazi nilizofanya ili kuongeza kipato ni kuwa mfasili wa kazi za Kiswahili kwenda Kiingereza kwa ajili ya kampuni kadhaa zilizokuwa na mikataba na vyuo kadhaa vya Marekani katika kukuza Kiswahili.

Kilichonisikitisha ni kwamba katika mradi huu, tulikuwa wafasili zaidi ya 20 wa Kiswahili kutoka nchi mbalimbali; lakini mimi ndiye pekee niliyekuwa Mtanzania. Wengine walitoka Kenya, Afrika Kusini, Canada na Congo.

Wanaosafiri kwa ndege za KQ – Shirika la Ndege le Kenya – wamekuwa wanasikia Kiswahili chenye lafudhi na msamiati wa Kenya kwenye matangazo yao. Hata kwenye mitandao, Kiswahili ambacho kinaonekana kurasimishwa ni cha Kenya, si cha Tanzania.

Sisi tumetumia nguvu nyingi kung’ang’ania Kiingereza, ambacho watu wetu hawawezi kuzungumza vizuri kwa kuwa hawakupata msingi mzuri wa kufunzwa lugha hiyo; ingawa imetumika kama lugha ya kufundishia masomo mengine tangu sekondari hadi chuo kikuu.

Ndiyo, Kiswahili ni lugha ya taifa tangu 1961. Watanzania wengi wanazungumza Kiswahili. Vyombo vyetu vya habari vingi, vinaandika au kurusha taarifa za habari na matangazo kwa Kiswahili.

Tuna BAKITA, Baraza la Kiswahili la Taifa. Tuna TUKI, Taasisi ya Ukuzaji wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo nasikia imekua na kujitanua zaidi.
Tuna miradi mingi ya kukuza Kiswahili. Lakini tumejifanya wanyonge wa kuenzi Kiswahili. Wakenya sasa wanaelekea kupora lugha yetu. Tusipostuka, kuna wakati tutajikuta tunakwenda Kenya kujifunza Kiswahili.

Natambua kuwa mjadala juu ya lugha ya kufundishia katika shule zetu haujaisha. Wapo wanaotaka Kiingereza kiendelee kutumika kufundishia watoto wetu. Wengine wanasema Kiswahili kitumike.
Hoja hiyo itajadiliwa siku nyingine. Lakini lililo wazi ni kwamba, lolote tutakaloamua halitakuwa na uzito, halitatekelezeka, iwapo litakosa msukumo wa kisiasa.

Kwa sasa, hatuna mwingine wa kubeba jukumu hili, bali Rais Magufuli. Alibebe kwa kuazimia na kuonyesha kwa vitendo kuwa popote atakapokuwa, atahutubia kwa Kiswahili ili kukidhi matakwa haya na kuepusha adha niliyotaja hapo awali.

Hatua hii itasaidia kuongeza ajira. Watahitajika wafasili. Yeye azungumze, wengine watafsiri, dunia isikilize.

Kwetu, au kwa yeyote anayejua lugha hiyo, Kiswahili ni hazina. Ni soko la ajira. Ni mtaji. Lakini hakijaweza kutumika kiuchumi kuboresha maisha ya wananchi kwa sababu viongozi wanakipuuza.
Inasikitisha zaidi kwamba marais wetu wameshindwa kukuza Kiswahili katika ngazi ya kimataifa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mwandishi na mzungumzaji mahiri wa Kiswahili na Kiingereza. Lakini alitumia Kiingereza kila alipohutubia jamii ya kimataifa.
Marais Ali Hassan Mwinyi, na Benjamin Mkapa nao walifuata nyayo za Mwalimu Nyerere. Walihutubia kwa kusoma hotuba walizoandika au walizoandikiwa na wasaidizi wao – kwa Kiingereza sanifu.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top