Serikali imeunda kikosi kazi kinachohusisha taasisi nyeti nchini kuchunguza sakata la kukamatwa kwa raia wawili wa Uholanzi wakiwa katika harakati za kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.
Kikosi
hicho kinaundwa na maofisa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Kikosi cha
Kupambana na Ujangili.
Kamanda
wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa aliwathibitishia
wanahabari jana kuundwa kwa kikosi kazi hicho na kwamba, upelelezi wa
sakata hilo umepamba moto.
“Upelelezi
ndiyo kwanza bado mbichi, kwa hiyo siwezi kusema lolote kama lini
watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa sababu upelelezi uko chini ya
kikosi kazi hicho,” alisema Mutafungwa.
Juzi
saa tano asubuhi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe, alitembelea Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (Kia) kushuhudia wanyama hao.
Profesa
Maghembe alisema kama kila kitu kitakwenda vizuri katika upelelezi,
watuhumiwa wa kosa hilo watafikishwa mahakamani siku ya Jumanne.
Wanyama
hao walikamatwa usiku wa kuamkia juzi katika uwanja huo wakati raia
hao, Artem Alik Vardanyian (52) na Eduard Alik Vardanyian (44) wakiwa
katika harakati za kuwasafirisha kwa kutumia ndege kubwa ya mizigo.
Hata
hivyo, raia hao wa Uholanzi walikuwa na vibali vilivyotolewa na
Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Charles Mulokozi ambaye
tayari amesimamishwa kazi kwa kashfa hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )