TIMU ya Simba imeshika uongozi wa Ligi Kuu baada ya kuifunga Mbeya City kwa mabao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba imezipiku Yanga na Azam FC zilizokuwa katika nafasi ya kwanza na pili kwa kufungana kwa pointi 47 baada ya wenyewe kufikisha pointi 48 licha ya kucheza mechi moja zaidi ya timu hizo mbili. Yanga na Azam FC juzi zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika kwenye uwanja huo.
Katika mchezo wa jana, Simba waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 72 lililofungwa na Daniel Lyanga baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Awadhi Juma. Wenyeji Simba walipata bao la pili baada ya mchezaji wa Mbeya City, Hassan Mwasapili kujifunga katika dakika ya 90 baada ya kutokea piga nikupige katika lango la timu hiyo.
Mbeya City ndio walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Simba katika dakika ya tano tangu kuanza kwa mchezo huo, ambapo Ditram Nchimbi nusura afunge lakini alipiga mpira nje. Simba walikaribia kufunga katika dakika ya sita na 12 wakati Ibrahin Ajib na Hamisi Kiiza walipokosa mabao baada ya kazi nzuri ya kipa wa Mbeya City, Hannington Kalyesebula kuokoa.
Katika dakika ya 32 Haruna Shamte nusura afunge kwa mpira wa adhabu lakini shule lake liligonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Simba. Mbeya City walifanya shambulizi jingine katika dakika ya 43 lakini juhudi za kipa wa Simba, Vicent Agban zilizuia upatikanaji wa bao hilo baada ya kufanya kazi nzuri ya kuokoa.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu. Katika dakika ya 66 Mbeya City walifanya mashambulizi kadhaa ya nguvu langoni mwa Simba, lakini hayakuzaa matunda. Raphael Alpha nusura aifungie Mbeya City bao katika dakika ya 72, lakini mpira wake uliokolewa na kipa wa Simba, Angban.
Simba: Vicent Angban, Emery Nimuoboma, Mohamed Hussein, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justine Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza/Awadhi Juma, Ibrahim Ajib na Brian Majengwa/ Daniel Lyanga.
Mbeya City: Hannington Kalyasebula, Hassan Mwasapili, Abubakar Shaban,Tumba Sued, Haruna Shamte, Kenny Ally, Raphael Alpha, Haruna Moshi `Boban’/Them Felix, Geofrey Mlawa, Joseph Mahundi na Ditram Nchimbi/Ramadhani Chombo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )