Wakati
joto la kuundwa Baraza la Mawaziri Zanzibar likiwa linaendelea kupanda
bila ya Chama cha Wananchi (CUF) kuwamo katika serikali, Katibu Mkuu wa
chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, leo anatarajiwa kutoa mwelekeo wa
kisiasa wa chama chake baada ya kususia uchaguzi mkuu wa marudio
visiwani humu.
Msimamo
huo wa CUF kuhusu mwelekeo wa Chama baada ya kugomea uchaguzi mkuu,
unakuja baada ya kukamilika vikao vizito vya chama hicho kikiwamo cha
Kamati Tendaji na Baraza Kuu la Uongozi vilivyofanyika Shangani Mjini
Zanzibar.
Akizungumza
toka mjini Zanzibar jana, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF,
Omar Ali Shehe, alisema kuwa tamko la chama hicho litatolewa na Katibu
Mkuu wa CUF baada ya kukamilika kwa vikao muhimu vya chama hicho.
Alisema
vikao hivyo vimefanyika kwa siku nne vikitanguliwa na vikao vya siku
mbili vya Kamati Tendaji vilivyofanyika chini ya Mwenyekiti wake, Maalim
Seif.
“Vikao
vimekamilika salama na ajenda kubwa tulikuwa tunajadili hali ya kisiasa
ya Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa marudio kinyume cha
Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Shehe.
Hata
hivyo, alisema maazimio ya kikao hicho yatatangazwa na Maalim Seif ili
wanachama na wananchi kwa jumla, wafahamu msimamo wa chama hicho.
Alisema
mwelekeo wa CUF kisiasa utaendelea kubakia kupigania haki ya wananchi
iliyoporwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim
Jecha, baada ya kufuta matokeo kinyume cha Katiba na Sheria Oktoba 28,
mwaka jana.
Aidha,
alisema Kikao cha Baraza Kuu kilikuwa cha kwanza kufanyika tangu
kilipopitisha azimio la chama la kususia uchaguzi mkuu wa marudio
uliyofanyika Machi, mwaka huu.
Msimamo
wa Baraza Kuu la CUF umesababisha chama hicho kupoteza viti vyote vya
Uwakilishi katika Majimbo 54 na Wadi 111 za madiwani katika Visiwa vya
Unguja na Pemba pamoja na kupoteza nafasi ya kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar.
Hata
hivyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,
alisema kuwa anaamini Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, atatumia
hekima na busara kwa kutumia nafasi zake 10 za Kikatiba kuwateua
viongozi wa vyama vingine kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa
madhumuni ya kuendeleza Serikali Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Hata
hivyo, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar iliyokuwa
ikishikiliwa na Maalim Seif, imekwama kufanyika uteuzi wake baada ya
vyama vilivyoshiriki uchaguzi wa marudio, kushindwa kufikia masharti ya
Katiba ikiwamo kupata asilimia 10 ya matokeo ya kura za Rais au viti vya
majimbo katika Baraza.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )