Siku chache baada ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), kufuta Tanzania kwenye nchi wanachama wake na hivyo kuikosesha serikali msaada wa zaidi ya Sh. trilioni moja kutokana na uchaguzi wa Zanzibar, Umoja wa Ulaya (EU), upo hatarini kutotoa Sh. trilioni 1.56 kwa sababu ya suala hilo huku mmoja wa Waziri wa Uingereza, akiitaka serikali yake isitoe Sh. bilioni 622 za msaada kwa Tanzania.
Kwa
mantiki hiyo, Tanzania ipo hatarini kupoteza jumla ya Sh. trilioni
2.182 kutoka EU na Uingereza endapo haitaridhishwa na suala la Zanzibar
linavyoendelea.
Tangu
Juni, 2014, Tanzania na EU ziliingia makubaliano ya msaada wa Euro
milioni 100 (sawa na Sh. bilioni 249), kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ya kiuchumi na kisiasa.
Kwa
mujibu wa ufafanuzi uliotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Siasa na
Habari, Luana Reale, EU imesikitishwa na namna uchaguzi wa marudio
Zanzibar ulivyofanyika Machi 20, mwaka huu, baada ya uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka jana.
“Tunarudia
wito wetu kwa serikali kuonyesha uongozi na kufanya mazungumzo ya pande
zinazovutana katika maoni ya kuhakikisha amani na umoja vinaendelea
kuwapo nchini,” alisema.
Alisema
Tanzania na EU wako katika makubaliano maalum ya utekelezaji wa miradi
kuanzia mwaka 2014 hadi 2020 iliyosainiwa Juni 2014, yenye thamani ya
Euro milioni 626 (Sh. trilioni 1.56), ikiwa ni wastani wa Euro milioni
100 (Sh. bilioni 249) kwa mwaka.
Alisema
kutoka kwa fedha na utekelezaji wa miradi husika, kunakwenda sambamba
na makubalinao maalum ya ushirikiano yaliyojikita katika maendeleo ya
kiuchumi na kisiasa.
“Maamuzi
juu ya ushirikiano wa maendeleo ikiwa ni pamoja na uamuzi wa mwisho wa
kiwango cha fedha yatachukuliwa kwa msingi wa matokeo ya mazungumzo,” alisema.
Hata hivyo, haikueleza moja kwa moja kama wataendelea kuchangia bajeti kuu kama ambavyo wamekuwa wakifanya kila mwaka wa fedha.
Uingereza
Waziri
wa zamani wa Ulinzi wanchi hiyo, Dk. Liam Fox, alililiambia Bunge la
nchi hiyo liinyime Tanzania Paundi milioni 200 ambazo ilitakiwa kutoa
kwa sababu ya sakata la uchaguzi wa Zanzibar.
“Walipa
kodi wa nchi za Magharibi wanategemea fedha zao kutumiwa kwa njia za
kimaadili..Sasa panapokuwa na ukiukwaji wa wazi wa haki za kisiasa au za
binadamu, watategemea majibu kutokana na misaada tunayochangia.
“Ukweli
ni kwamba Marekani imechukua hatua imara inatoa ishara nzuri…Tunapaswa
kuwa tunafanya mapitio ya mchango wetu katika hali kama hiyo,” alisema.
Uingereza
imekuwa ikifikia lengo lake la kutenga asilimia 0.7 ya pato lake kila
mwaka, kwa ajili ya msaada kwa nchi za nje kutokea mwaka 2013, baada ya
Idara kwa ajili ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), kufikia asilimia 32
kwa mwaka mmoja.
“Kuna sehemu nyingi duniani ambako tunaweza kuwa tunatumia msaada wetu kikamilifu kupunguza umaskini."
Kwa
upande wake, Waziri wa zamani wa Mazingira na Mbunge Mwandamizi kutoka
Chama cha Conservative, Owen Paterson, alisema DFID inapaswa kupunguza
misaada yake kwa Tanzania, sambamba na uamuzi wa Marekani.
“Wizara
ya Mambo ya Nje inasema uchaguzi si halali na tunaendelea kutumia fedha
zetu vilevile, hii haiwezi kuwa sawa,” alisema Paterson.
“Wamarekani wamekiri kuwa njia hii haiwezi kuwa sawa na wamechukua uamuzi na sisi tunapaswa kuchukua uamuzi hapo hapo,”alisema.
Hali Ilivyo
Wiki
iliyopita, Wizara ya Fedha na Mipango, ilieleza kuwa wahisani 10 kati
ya 14 waliokuwa wanachangia mfuko wa bajeti ya Serikali Kuu wamejitoa na
kuweka shakani upatikanaji wa Sh. trilioni 1.37 kwa bajeti ya mwaka huu
ambazo zilitarajiwa kutoka kwa wahisani.
Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Servacius Likwelile, alisema waliobaki ni
Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Dernmark na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Wahisani wengine wa bajeti ya Tanzania ni Uingereza, Canada, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway na Sweden.
Dk.
Likwelile alieleza kuwa kujitoa kwa wahisani hao kunatokana na
changamoto zilizopo katika nchi zao na kwamba mchango wa wahisani katika
bajeti ya mwaka 2014/15, ilikuwa trilioni moja, katika bajeti
iliyofuata ilishuka hadi Sh. bilioni 800
Chanzo:Nipashe
Chanzo:Nipashe
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )