Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad kesho ataelezea mwelekeo wake kisiasa, ikiwamo kufafanua kiundani uamuzi wa chama hicho kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
Mgombea huyo wa urais Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ataeleza mambo hayo ikiwa imepita takribani wiki moja tangu Baraza Kuu la chama hicho kutoa msimamo wake wa kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na wawakilishi na madiwani.
CUF kilisusia kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu baada ya Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani, akisema kulikuwapo na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaarifu kuwa mkutano wa kiongozi huyo utakuwa wa kwanza kwake, tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio na ataeleza mambo muhimu yatakayotoa picha halisi ya mwelekeo wake na CUF.
“Katika mkutano uliopita tamko lilikuwa la Baraza Kuu ila keshokutwa (kesho) Maalim Seif atazungumza kama Katibu Mkuu na aliyekuwa mgombea urais. Kuna masuala mengi atayaeleza kwa kina, hasa hili la uamuzi wa CUF kususia uchaguzi,”zilieleza taarifa hizo.
“Atazungumzia kwa kina uchaguzi ulivyokuwa na kujibu maswali ya watu wa kada mbalimbali waliokuwa wakihoji nini hatima ya CUF, baada ya kususia uchaguzi na hivyo kupoteza nafasi za uwakilishi.”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )