Rais wa Marekani Barack Obama amekiri kwa mara ya kwanza kwamba serikali yake ilifeli katika kutatua mzozo wa Libya.
Amesema hilo huenda ndilo “kosa kubwa” zaidi alilolitenda wakati wa utawala wake.
Bw Obama amesema Marekani haikua na mpango mahususi wa jinsi taifa hilo
litakavyotawaliwa baada ya kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar
Gaddafi.
Alisema haya katika mahojiano na runinga ya Fox News kuangazia mafanikio na mapungufu ya utawala wake.
Hata hivyo ametetea hatua ya kuingilia kijeshi nchini Libya. Marekani na
Muungano wa NATO zilitekeleza mashambulio ya anga kuwalinda raia baada
ya kuzuka maasi dhidi ya Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Lakini baada ya mauaji ya kiongozi huyo, Libya ilitumbukia katika vita
vya wenyewe kwa wenyewe kati ya makundi ya waasi huku makundi mawili
yakiunda serikali na mabunge tofauti.
Katika hatua za kurejesha utulivu serikali ya muungano wa kitaifa
inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imewasili katika mji mkuu Tripoli
ili kuanza mipango ya kuongoza nchi ya kurejesha hali ya kawaida.
Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika Novemba na Rais Obama
atakabidhi madaraka kwa mrithi wake Januari mwakani baada ya kuongoza
kwa mihula miwili.
Chanzo: BBC
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )