Uchunguzi wa kitalaam uliofanyika umebaini kuwa Shisha ina madhara kwa afya ya watumiaji hasa vijana na watoto. Watumiaji wa Shisha wanatumia kiwango kikubwa cha tumbaku kwa muda mfupi, hali inayoongeza madhara yatokanayo na tumbaku kama vile: – Saratani, Magonjwa ya Mapafu, Kibofu cha mkojo, Tezi dume, Koo, Mdomo na Kiywa, Ngozi, Ini, Ubongo.
Pia imebainika kwamba matumizi ya Shisha huambatana na kuongezewa dawa nyingine za kulevya na hivyo hufanya watumiaji wa Shisha kupata uraibu wa dawa za kulevya. Matumizi ya dawa hizo za kulevya ni kosa la jinai.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kurejea na kusisitiza agizo lake la tarehe 12 Machi 2015 la kuzuia matumizi ya sigara na matumizi ya bidhaa za tumbaku katika maeneo ya umma
Inakumbushwa kwamba agizo hili limezingatia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 T.L 2002, ya Sheria za Tanzania kipengele cha 12 (1) ambacho kinakataza matumizi ya Tumbaku katika Maeneo ya Umma.
Madhumu ya Agizo hili ni kuilinda Jamii kwa ujumla kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara. Wizara inawakumbusha wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya tumbaku. Aidha, agizo hili linaijumuisha jamii yote katika kubaini madhara ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia matumizi ya tumbaku katika maeneo ya kazi na maeneo yote ya umma.
Agizo hili linawahusu wananchi wote nchini wanaopata huduma katika maeneo ya umma kama ilivyotafsiriwa na sheria husika.
Matumizi ya tumbaku hayaruhusiwi katika maeneo yote ya umma. Maeneo haya yanajumuisha ofisi zote za Serikali na tasisi zake zote, watu binafsi, vyuo, vituo vya huduma za Afya zikiwemo Hospitali, vituo vya Afya na zahanati, vituo vya usafiri wa Anga, Mabasi, bandari na treni, sehemu za mikutano, mapumziko, bustani na fuko za maji,sherehe,michezo,masoko,maduka makubwa pamoja na sehemu za kuabudu.Na kwa mtu yeyote anayeendesha shughuli katika maeneo ya umma analazimika kutenga eneo maalum kwa ajili ya wavuta sigara.
Kwa kuwa Mhe. Waziri mwenye dhamana na masuala ya Afya nchini ameona hatari hii ya Uvutaji wa sigara na utumiaji wa bidhaa za tumbaku kwa afya ya Wananchi, kuanzia leo tarehe 4/7/2016 matumizi ya Shisha nchini yamepigwa marufuku kwa wote wanaojihusisha na matumizi hayo, na kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na upatikanaji wa Shisha nchini
Hivyo basi, kwa agizo hili katika maeneo yote nchini ambako matumizi ya Shisha hufanyika ni marufuku matumizi hayo kuendelea kutumika.
Aidha vyombo vya Dola na mamlaka husika vinahimizwa kusimamia kwa ukamilifu katazo hili.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )