Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi ujao wa
mwaka 2020 kwa kuboresha daftari la wapiga kura ili kuweka taarifa za
walengwa wakiwemo watakaopiga kura baada ya kufikisha umri wa kupiga
kura.
Aidha,
itawahusu walioshindwa kupiga kura katika chaguzi zilizopita kutokana
na sababu mbalimbali. Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Ofisa Uchaguzi
wa Tume hiyo, Adam Nyando wakati akikabidhi taarifa za Uchaguzi Mkuu wa
2015 kwa mkoa wa Pwani.
Alisema,
baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2015, wameanza maandalizi ya
uchaguzi mkuu ujao na si kwamba kwa sasa Tume imelala.
“Watu
wanafikiri uchaguzi ukishaisha ndio kazi imekwisha kumalizika kwa
uchaguzi mmoja ni maandalizi ya uchaguzi ujao kwani kwa sasa tunaendelea
na uboreshaji wa daftari la wapigakura pamoja na kura za maoni,” alisema Nyando.
Alisema
uchaguzi uliopita ulikwenda vizuri na hakukuwa na matatizo makubwa
licha ya matumizi ya mfumo mpya wa BVR, lakini matokeo yake umekuwa
mfumo mzuri na umepata mafanikio makubwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, akizungumza alitumia fursa hiyo
kuwapongeza Watanzania kwa kufanya uchaguzi mzuri usiokuwa na vurugu
wala uvunjifu wa amani.
Ndikilo
alisema nchi nyingine kipindi cha uchaguzi ni kipindi kibaya cha
uvunjifu wa amani, ikiwa ni pamoja na umwagikaji mkubwa wa damu, hasa
kwa pande zisizokubaliana matokeo.
“Uchaguzi
ulienda vizuri licha ya changamoto zilizojitokeza za hapa na pale
lakini watu walivumiliana na kukubaliana na matokeo kilichobaki sasa ni
kufanya kazi ili kuwaletea maendeleo wananchi, kikubwa ni tume kufanyia
kazi changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na usafiri na
ucheleweshwaji wa matokeo kwa baadhi ya sehemu,” alisema Ndikilo.
Akikabidhi
taarifa hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ofisa Uchaguzi wa mkoa, Shangwe
Twamala alisema mkoa huo umepata nakala 47 ambazo zitasambazwa kwa
wadau mbalimbali wa uchaguzi.
Alisema
taarifa hizo zitasambazwa kwenye ofisi za mkuu wa mkoa, wakuu wa
wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji na wilaya na taasisi za elimu
ya juu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )