Mbowe na Edward Lowassa |
Vyanzo vyetu kutoka serikalini na CCM vinaeleza kuwa, miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuwatia hofu wafuasi wa Chadema wanaojipanga kujitokeza kwenye maandamano na mikutano inayoandaliwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu.
Mikutano na maandamano hayo yanafanywa chini ya mwamvuli wa operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (UKUTA), jambo ambalo linapingwa na Rais John Magufuli pamoja na Jeshi la Polisi.
Tayari utekelezwaji wa mkakati huo umeanza, ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa hatohudhuria mikutano na maandamano hayo na atakimbilia nje ya nchi.
“Jambo la mikutano na maandamano lipo kikatiba na kiukweli kuzuia ni kukiuka Katiba, jambo linalofanyika ni kujaribu kuwagawa watu.
“Kibaya zaidi ni kuwa, rais kapiga marufuku jambo ambalo hakupaswa kufanya hivyo. Hapa ndipo ugumu unaonekana maana kuna katiba na kauli ya rais inayotoa maelekezo yanayopingana na Katiba,” kinaeleza chanzo hicho kutoka CCM.
Kwa sasa, taarifa zilizopo kwenye mitandao ya jamii zinamtuhumu Mbowe kutaka kutorokea nje ya nchi ili kukwepa kushiriki maandamano na mikutano ya Ukuta iliyopigwa marufuku na Rais Magufuli na polisi.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Mbowe amepanga kusafiri nje ya nchi tarehe 28 Agosti mwaka huu ikiwa ni siku tatu kabla ya kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo.
Taarifa hizo zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii, zimeambatanishwa na kile kilichodaiwa kuwa ni tiketi ya safari hiyo zinadai kuwa, Mbowe anapanga kusafiri ili kukimbia vurugu zitakazotokea Septemba Mosi mwaka huu katika maandamano hayo.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa imeeleza kuwa, ujumbe huo hauna ukweli wowote na kwamba, sababu za kusambazwa kwa ujumbe huo ni nia ovu ya wanaopinga maandamano hayo.
“Mheshimiwa Mbowe yupo mstari wa mbele na anaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha maazimio ya Kamati Kuu juu ya uanzishwaji na utekelezaji wa operesheni ya Ukuta inafanyika kwa ufanisi.
“Mpaka sasa mwenyekiti anaendelea na vikao vya kimkakati ndani ya Kanda ya Kaskazini kama ilivyopangwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, kile kinachoelezwa kama tiketi ya safari ya ndege ya Mbowe, kimetengenezwa kwa kutumia kompyuta na hakina uhalisia na kusisitiza kuwa Mbowe atashiriki kikamilifu.
Mbali na mkakati huo wa kutengeneza propaganda kuwa viongozi wa kitaifa wa Chadema hawatakuwepo nchini katika siku iliyopangwa kwaajili ya mikutano na maandamano hayo, Jeshi la Polisi kote nchini, linaendelea kukamata watu wote wanaovalia fulana zenye neno; ‘UKUTA’.
Jeshi hilo ambalo limesharipotiwa kukamata watu mbalimbali katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Mwanza, limeanza pia mkakati wa kufanyisha mazoezi vikosi vyake na kuwaita wanahabari ili waonyeshe mazoezi hayo kwa lengo la kuwatisha wananchi ambao huenda wakashiriki maandamano hayo.
Vikosi vya kutuliza ghasia (FFU), vimekuwa vikialika wanahabari ili kuonyesha mazoezi yanayodaiwa ni ‘kujiweka tayari kukabili uvunjifu wa amani’, Polisi wanaamini kwa kufanya hivyo, wananchi wengi wataogopa kujitokeza katika maandamano ya UKUTA.
CCM pia, imetumia mbinu ya kuwataka vijana wa chama hicho (UVCCM) kutangaza kufanya maandamano nchi nzima, siku moja kabla ya maandamano ya Chadema ili Polisi watangaze kuzuia maandamano hayo na kutengeneza dhana kuwa polisi hawapendelei chama chochote!
Mbinu hii ilitumika pia mwezi Juni, mwaka huu baada ya Chadema kutangaza kufanya mikutano nchi nzima na kisha, Christopher Ole Sendeka, msemaji wa CCM kutangaza kuwa CCM pia itazunguka nchi nzima kufanya mikutano ya kuikabili Chadema.
Jeshi la Polisi lilitumia mwanya huo kudai kuwa, mikutano ya vyama hivyo (CCM na Chadema) itasababisha vurugu na uvunjifu wa amani na hatimaye kuipiga marufuku lakini lengo hasa likiwa ni kuzuia mikutano ya Chadema.
Chanzo:Mwanahalisi
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )