Kuna
baadhi ya magazeti na mitandao imekuwa ikiandika kuwa Dkt. Kigwangalla
amesoma high school na aliyekuwa 'Tabibu', Ndg. Juma Mwaka, shule ya
Kigoma Sekondari na kwamba walikuwa marafiki; hizi ni habari za uongo,
za kupika zenye kupotosha ukweli ili kuwaaminisha watu kuwa 'wanajuana'
na pengine wana ugomvi 'binafsi'.
Nimekuwa
nikimpuuza kwa sababu sikuwa na haitotokea nikawa na nia mbaya dhidi ya
mtanzania mwenzangu yeyote kwa sababu tu mimi nina dhamana ya uongozi.
Sinaga tabia hiyo.
Uongo
ukirudiwa rudiwa hubadilika na kuwa ukweli. Leo nimeamua, hapa chini,
kukanusha ili watanzania pia mumpuuze, tuendelee kuimarisha huduma za
tiba asili na tiba mbadala kutoka kwa matabibu wa kweli wanaofuata
taratibu na siyo wasanii kama huyu. Uongo ama uzushi dhidi yangu mimi
binafsi kamwe hautonirudisha nyuma mimi kama mtumishi wa umma. Lazima
ifike mahali tujenge nchi ya watu 'serious' wanaofuata Sheria, Kanuni na
Taratibu. Wanaoheshimu Serikali. Kwenye Afya za watanzania hatuwezi
kuvumilia usanii, lazima tuwalinde walaji. Hili ni jukumu tulilopewa na
Mhe. Rais. Tutasimamia Sheria ipasavyo. Hatutolegeza hata kidogo.
1.
Sikusoma 'high school' Kigoma Sekondari. Nimesoma O'level (form I - IV)
Kigoma Sekondari. High School nilisoma Shinyanga Sekondari. Sikumbuki
kusoma katika shule zote hizi mbili na mtu mwenye Jina Hilo. Kama
alisoma Kigoma Sekondari labda mbele yangu ama nyuma yangu. Pia kipindi
nasoma Kigoma Sekondari, hakukuwa na 'high school'.
2.
Ndg. Juma Mwaka hajawahi kuwa rafiki wala adui yangu. Sina ugomvi
binafsi. Nafanya kazi ya kusimamia Sheria ya tiba asili na tiba mbadala
ipasavyo.
3.
Naithamini tiba asili na tiba mbadala na Ndiyo maana nimeongoza Wizara
ya Afya kufanya Mapinduzi makubwa kwenye eneo hili, ikiwemo kuweka
utaratibu mzuri na rahisi zaidi wa kusajili watoa huduma, dawa zao,
mazingira wanapotunzia dawa, wasaidizi wao, viwanda vyao, na pia kuweka
mikakati ya uanzishwaji wa viwanda vya dawa za tiba asili na tiba
mbadala sambamba na kufanyia utafiti dawa zao na kudhibiti ubora wa dawa
zenyewe na dozi wanazowapa wateja.
4.
Muulizeni Ndg. Juma Mwaka anaposema ana ugomvi 'binafsi' na mimi,
anamaanisha nini, ugomvi upi? Juu ya nini? Awape taarifa kamili. Mimi
Sina ugomvi naye. Kwanza sikuwahi kumjua kabla ya ziara yangu ya kikazi
pale Foreplan, ntakuwaje na ugomvi na mtu nisiyemjua? Si utakuwa ujuha
huo?
5.
Mnaofuatilia suala hili mtakeni Ndg. Juma Mwaka awape majibu ya Msingi
ya hoja za wakaguzi kutoka Wizara ya Afya. Mimi nilikuwa msimamizi
nikiwapa nguvu wataalam wafanye kazi yao. Wataalamu walikuwepo, nao ana
ugomvi nao 'binafsi'? Mwambieni awajibu kama dawa za tiba ya kisasa
kukutwa kwenye eneo lake la kazi ilikuwa halali? Alikuwa na vibali vya
kutunza zaidi ya maboksi 200 ya dawa? Alikuwa na vibali vya kutunza
zaidi ya magunia 10 ya dawa za tiba asili na tiba mbadala baada ya
kufutiwa usajili? Alikuwa na uhalali wa kuendelea kutangaza kwenye
vyombo vya habari kuwa wateja wake wafuate dawa pale ili wasikatishe
dozi? Tena kinyume na katazo la Baraza la tiba asili na tiba mbadala!
Yeye yuko juu ya Serikali? Yuko juu ya Sheria? Ama anadhani anaweza
kuidhihaki na kuiogofya Serikali?
6.
Baada ya ziara yangu ya December 2015, ambapo sikutoa maelekezo ya
kumfungia wala kumfutia kibali, niliwaelekeza Baraza la Tiba Asili na
Tiba mbadala kuwa wawaite wawaelekeze matabibu wote wafuate Sheria,
kanuni na taratibu. Waliitwa. Wakaelekezwa. Waungwana wakatii. Yeye
hakutii, wakamfuta. Baada ya kufutiwa usajili, akaendelea kujitangaza na
kutoa huduma, yeye ni nani?
7.
Kufanya haya ni kuvunja sheria za nchi. Na makosa haya yana adhabu
zake. Sisi kama Serikali tumeagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi
yake. Serikali ina mkono mrefu, itamkamata. Itamtia nguvuni na
atafikishwa mahakamani. Ataenda kujitetea huko kuwa ana 'ugomvi binafsi'
na Naibu Waziri Kigwangalla!
Mwisho,
aende akafuatilie kisa cha mfanyabiashara wa kigiriki aliyesema
ameiweka Serikali mfukoni - Mwalimu Nyerere alimfanya nini!
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )