Hadi wiki mbili zilizopita, Ruby na Clouds walikuwa wakisafiri kwenye boti moja. Kama ilivyokuwa kwa wasanii waliopata ‘usajili’ wa kutumbuiza kwenye tamasha la thamani la Fiesta mwaka huu, Ruby naye alijimwaya mbele ya kadamnasi kuweka sahihi kwenye mkataba. Kushoto kwake B12, kulia kwake Hamza Balla mwakilishi wa Tigo, wadhamini wa tamasha hilo na kila mmoja tabasamu na bashasha zikiwa zimewajaa nyusoni – deal done!
Heee! Yametokea wapi tena ya Ruby kususia show hiyo licha ya kusaini mkataba? Ya kwamba Clouds walitoa ofa kiduchu isiyotosha hata kumwezesha kufanya maandalizi yake binafsi? Mkataba alikuja kuusoma baada ya kuusaini? Makubwaa!
Ruby kageuka mada mtandaoni, maneno yamemtoka akitupa shutuma nzito kwa uongozi wake wa THT kuwa haujali. “To be honest naumia sana sababu they don’t care,” alisema Ruby kwenye mahojiano na Tizneez.
“So if someone hakujali, what can you do? Tatizo ndio kama hilo unakuwa na management ambayo haijali maslahi yako kwenye maisha yako. Tunajikuta tunakuwa na management ambazo zinajali umabavu, zinaendesha wasanii kimabavu kuliko kiakili ya kutimiza malengo ya wasanii wao ambapo sisi wasanii wa kike tunaonewa sana. Unadhani kwanini Lady Jaydee wanamuita komando?” alihoji.
Mimi na wewe hatuna nafasi ya kujua kilichopo nyuma ya pazia. Maneno yawe ya ukweli ama yawe na chumvi kiasi, tunachoweza kunusa baada ya kauli nzito ya Ruby ni yale yanayoweza kujiri baadaye.
Kwa msanii mchanga kama Ruby kuingia kwenye vita na himaya ya Clouds Media ni sawa na panzi na ndege tai kuingia vitani – wajua tu nani ataweka silaha chini. Ruby amemtukana mamba ilhali hajaufikia hata robo mto anaojaribu kuuvuka.
Njia aliyoitumia kufikisha malalamiko yake inaweza kumponza kwa kiwango kisichoelezeka – iwapo hana back up ya kutosha. Ni kwasababu bado hajafika katika hatua ambayo hata kama vituo vya Clouds vikimweka kwenye ‘orodha nyeusi’ ataweza kuhimili kulisukuma gurudumu la muziki wake. Najua utasema ‘ahhh, mbona inawezakana’ – Ndiyo inawezekana, lakini labda uwe Lady Jaydee!
Sina mfano mwingine ninaoweza kuutaja wa mtu aliyewahi kupishana nao hao jamaa na akaendelea kuwika kwenye kila kona ya spika za redio zinazolia mtaani. Ruby ana kipaji, anaimba sana, ana sauti inayoweza kumtoa nyoka pangoni, lakini haina faida sana kuingia vitani na waliompandisha, zaidi tu, itamuumiza.
Na kiukweli, Ruby asingekuwa na walau jina hilo alilonalo sasa kama Clouds FM/TV isingetumia nguvu hiyo iliyotumia kumfanya awe ‘relevant.’ Unakumbuka kuna kipindi sauti ya Ruby ilikuwa inasikika mara kadhaa kila baada ya saa Clouds FM na TV, si tu kwa kucheza wimbo wake, bali jingles za station. Kiukweli mimi hadi ilinikera!
Ilitumika nguvu kubwa kuufanya ‘Na Yule’ uwe hit song hadi redio zingine zikaupokea na kuanza kuucheza pia. Leo hii kwa msanii kama huyu kuja kuongea maneno kama yale, inamfanya awe mkosaji zaidi hata kama akionesha huruma kiasi gani. Ni sawa na mzazi aliyejinyima mengi kumsomesha mwanae kwa tabu ili ampatie elimu itakayomsaidia katika maisha yake.
Ndio, anaweza kuwa amekosewa mno na uongozi wake, lakini kuna namna alitakiwa kuwasilisha nung’uniko lake na kuyamaliza kama ndugu. Kama tu vile ambavyo mzazi akimkosea mwanae!
Muziki wa leo kipaji pekee hakitoshi. Unahitaji nguvu nyingi za nyuma ya pazia na fitina nyingi. Na kwakweli, itamhitaji nguvu nyingi zaidi Ruby kuweza kufika katika daraja la wasanii kama Vanessa Mdee, Shaa na wengine akifanya kazi bila ya nyimbo zake kuchezwa na vituo vya Clouds. Bado hajafika hapo, ana safari ndefu sana.
Bila shaka wanaweza kuyamaliza.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )