Featured
Loading...

VIJIJI 49 BUMBULI KUPATA UMEME AWAMU YA TATU YA MRADI WA UMEME VIJIJINI

 
janu1
January Makamba Mbunge wa jimbo la Bumbuli mkoani Tanga
…………………………………………………………………………………………………
Raisa Said, Bumbuli
Jumla ya vijiji 49 vya Halmashauri ya Wilaya vitapata umeme katika awamu ya tatu ya Mradi ya Umeme Vijijini ambayo imeanza hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika halmashauri hiyo jana, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba aliishukuru serikali kwa kupeleka umeme katika hivyo na kusema kuwa hatua hiyo inafanya vijiji vyote 90 vya halmashauri hiyo kufikiwa na umeme baada ya awamu hiyo.
Makamba,ambaye pia ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na Masuala ya Muungano alisema kuwa vijiji 50 vilipata umeme kupitia mradi wa umeme vijijini katika awamu ya kwanza na ya pili.
“Tunakushukuru Waziri na serikali kwa ujumla kwa kuwapatia umeme wananchi wa Halmashauri ya Bumbuli,” alisema.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, Professor Sospeter Muhongo amesisitiza juu ya umuhimu wa kupanga na kutekeleza mpango wa umeme vijijini kwa kuangalia kupanuka kwa matumizi katika kipindi cha muda mrefu.
Professor Muhongo ambaye yuko katika ziara mkoani Tanga kuangalia maendeleo ya shughuli za mradi wa umeme vijijini, aliyasema hayo katika kijiji cha Mbuzii, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, wilayani Lushoto mara baada ya kukagua mashine ya kupozea umeme ya KVA 50 kijijini hapo.
Alikuwa anataka kujua kama mashine hiyo itatosheleza kuwadumia wananchi wa eneo hilo kama idadi ya watumiaji ikiongezeka.
Waziri huyo aliambiwa na mashine hiyo itatosha kwa wakazi wapatao 1000 waliopo hapo kwa muda huu na baada ya miaka miwili mitatu itabidi iwewekubwa zaidi ili kuhudumia watu wengi zaidi.
“Tusifanye kazi ya mara mbili mbili. Tunapoweka miundo mbinu hii lazima tulenge matumizi ya miaka mingi hadi miaka 50,” alisema.
Alisema kuweka miundombinu isiyoangalia matumizi ya uda mrefu siyo busara kwani hakuna hakika kuwa hiyo miaka miwili au mitatu watumiaji wakiongezeka kutakuwa na fedha za kununulia na kuweka mashine hizo. Alitaka utekelezaji wa Umeme Vijijini awamu ya tatu ambayo ytayari imekwisha anza kuzingatia suala la kuweka miundombinu ambayo itatumiwa kwa muda mrefu bila kubadilisha.
Professor Muhongo aliwataka wananchi wa vijijini kujiandaa kubadilisha uchumi wana maisha yao kutokana na azma ya serikali kupelekea umeme mwingi vijijini.
“Tunaleta umeme mwingi vijijini kwa sababu tunataka mabadiliko ya uchumi na ndiyo maana serikali imeweka bajeti ya Sh. Trilioni moja kwa mwaka kupeleka umeme vijijini na kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme Tanzania kutoka asilimia 40 ya hivi sasa hadi asilimia 75,” aliwaeleza wakazi wa Bumbuli.
Profesa Muhongo alisema kuwa Tanzania haiwezi kujivunia mamendeleo wakati kuna watu bado wanatumia kibatali kwa ajili ya taa.
Hata hivyo, Waziri huyo aliwataka watanzania kuwa wavumilivu na subira kwa sababu vijiji vyote 15,000 nchini haviwezi kupata umeme wakati mmoja. “Hata kule kwenye jimbo langu, au hata anakotoka Rais, au Waziri Mkuu kuna vijiji ambavyo havitajapata umeme. Tuwe wavumilvu ndugu zangu kwa sababu serikali imeazimia kuleta umeme kwa watanzania wote,’ alisema.
Alieleza kuwa wakati wa Bumbuli na maeneo mengine vijijini kujiandaa kuchakatua bidhaa zaona badala ya kuuza bidhaa ghafi. “jiandaeni kuuza unga badala ya mahindi au kuuza matunda yaliyokwisha kuchakatuliwa na kufungwa kitaalamu moja kwa moja kwenye maduka ya vyakula makubwa badala ya mahindi au matunda ghafi,’ alisema.
Akijibu swali moja aliloulizwa na mwananchi mmoja juu ya taratibu za kupata umeme kwenye makazi, aliiagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutembelea maeneo yote ambayo yameletewa umeme au yana matarajio ya kupelekewa umeme ili kuwaelezana kuwaelekeza wananchi juu ya taratibu za kujiunganisha na umeme.
Shirika hilo litakuwa na ziara august 25, mwaka huu katika vijiji vya Bumbuli kujibu na kuelekeza kuhusu masuala mbalimbali ya taratibu za umeme.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top