Huyu ni aina mojawapo ya chura
ambaye hapatikani mahali popote duniani isipokuwa katika Hifadhi ya
Mazingira asili ya Mkingu ambaye ni mojawapo ya kivutio cha utalii
katika hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na
Utalii)
Baadhi ya sehemu za kuvutia katika
Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo ni njia mojawapo
inayotumiwa na watalii kwenda kijiji cha Maskati kuangalia vivutio vya
Utalii vinavyopatikana katika Hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela-
Wizara ya Maliasili na Utalii)
Maporomoko Lusingizo yenye mita
zaidi ya 50 yaliyoko katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo
ni mojawapo ya kivutio cha Utalii katika Hifadhi hiyo, Hadi hivi sasa
kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha umeme katika kivutio
hicho cha utalii. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na
Utalii)
………………………………………………………………………..
Hifadhi asili ya Mkingu ipo
wilaya ya Muvemero Mkoani Morogoro. Hifadhi hii ni eneo muhimu sana
kiutalii kutokana na upekee wake wa maisha ya viumbe, mimea pamoja na
maisha ya binadamu kiujumla.
Hifadhi hii ina ukubwa wa hekta 26, 334 na imezungukwa na vijiji vitano ambavyo vipo ndani ya kata sita na tarafa mbili.
Tangu kuanzishwa kwake Hifadhi
hii mwaka 2016, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii
chini ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) imekuwa
ikihudumia hifadhi hii kutokana na kuwa na mimea na viumbe ambavyo ni
vivutio pekee vya Utalii nchini ambavyo havipatikani mahali popote
duniani.
Mhifadhi Mkuu wa Mazingira asili
ya Mkingu, Bw. Abeid Kindo anasema kutokana na sifa hizo za kipekee
zinazopatikana katika Hifadhi hiyo imekuwa na umuhimu wa aina mbili
ambao ni umuhimu wa kidunia na umuhimu wa kitaifa, Katika umuhimu wa
kidunia upo katika viumbe, mimea na wanyama.
Anasema hifadhi hii ina wanyama
wenye uti wa mgongo 392 kati ya hao 32 hawapatikana mahali popote
duniani isipokuwa ni Mkingu tu yaani ni endemic species. Aidha ,
alisema kuna vyura na ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo tu.
Bw. Kindo anasema kuwa hifadhi
hiyo imejaliwa kuwa na wanyama wanaotambaa 42 kati ya hao 14
hawapatikanimahali popote duniani isipokuwa Mkingu tu pamoja na aina
ya ndege 214 kati ya hao ni aina nne ndio wanaopatikana katika hifadhi
hiyo.
Mbali na hiyo, Anasema kuwa ndani
ya hifadhi kuna msitu unaotumika kwa masuala ya mila za Waluguru kuwa
eneo hilo ni zuri sana amabalo nalo ni kivutio cha utalii ndani ya
msitu huo
Mbali ya kupatikana kwa wanyama
na mimea katika Hifadhi hiyo Bw, Kindo anaeleza kuwa kuna pango la
Malolo ambalo wenyeji wa Mkindo wana historia kubwa ya pango hilo
ambalo wenyeji hawataweza kusahau kwani kuna mwanaume mmoja aliiba mke
wa Mtu akaishi naye ndani ya pango hilo kwa muda wa miaka 3 bila
kujulikana kijini. Pango hilo lina vyumba mithili ya nyumba iliyojengwa.
Pia anasema kuwa nadni ya
hifadhi hiyo kuna pango ambalo ukikaa nje kuna upepo unaotoka ndani
unapuliza hiyo ni ishara tosha kuwa humo ndani ndani kuna uhai.
Anabainisha kuwa hifadhi hiyo ina
jiwe lenye alama za nyayo za binadamu, kwato za mifugo ikiwa hiyo ni
ishara tosha kuwa maisha ya kale ya binadamu yalianzia ndani ya hifadhi
hiyo. .
Aliongeza kuwa mbali ya mapango
ndani ya hifadhi hiyo , kuna maporomoko Lusingizo yenye mita zaidi ya 50
, hadi hivi sasa kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha
umeme katika kivuto hicho cha utalii.
Pia kuna magofu ya kale ya
Wajerumani ambayo waliishi ndani ya hifadhi kabla vita vya pili vya
dunia na baada ya kuondoka kwa Wajerumani ilikuwa shule ya msingi ya
kijiji cha Mafuta, na baada ya eneo hilo likatangazwa kuwa hifadhi ,
Shule ile ilitolewa na kujengwa kijijini.
Bw. Kindo anasema licha ya hifadhi
hiyo kuwa na vivutio lukuki bado imekuwa ikitembelewa na idadi ya
watalii isiyoridhisha licha kwa mwaka jana wameweza kupata watalii
75 kutoka Ujerumani,
‘’Tokea mwaka jana hadi hivi sasa
tumeweza kuibua vivutio saba vya utalii na tunaendelea kufanya
jitihada za makusudi ili kuhakikisha tunakuwa na vivutio vingi vya
utalii ili tuweze kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi ‘’.alisema
Bw. Kindo
Aidha,Alisema Hifadhi hiyo ndio
chanzo cha mto Wami, mto Ruvu na Mto Mkingu ambapo maji hayo yamekuwa
yakitumika katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo,uvuvi,mazalia na
makazi ya mimea na wanyama bila kusahau maji hayo ndiyo hutumika
kuwanyesha wakazi wa Dare s Salaam na mikoa ya jirani
Amewataka wanafunzi wa vyuo
mbalimbali wasisubili watafiti kutoka nje ya nchi kwenda kufanya tafiti
katika Hifadhi hiyo badala yake wao wawe mstari wa mbele katika
kuvumbua vitu vingi ambavyo vinapatikana katika hifadhi hiyo
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )