Featured
Loading...

Watumishi wanafunzi hewa kusakwa vyuoni


MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ameunda Kamati ya wataalamu wa mkoa na kuiagiza kupita kwenye vyuo vya elimu ya juu ili kuhakiki ‘wanafunzi hewa’ ambao ni watumishi wa serikali kutoka mkoani humo, wanaodaiwa kuwa na ruhusa kusoma kwenye vyuo hivyo.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Sumbawanga jana, Zelothe alisema uhakiki wa watumishi hewa bado ni kaa la moto na kwamba hakuna jiwe litakalobakizwa bila kugeuzwa katika utaratibu huo.

“Nimeunda Kamati ya wataalamu wa Mkoa tayari wameanza kutembelea vyuo vya elimu ya juu nchini ili kuhakiki, kuonana ana kwa ana na watumishi wa umma kutoka mkoani hapa wanaosoma kwenye vyuo hivyo, pia kupata taarifa zao kutoka kwa wakuu wa vyuo hivyo. “Nina uhakika watumishi wengi wa umma kutoka mkoani kwetu hawapo kwenye vyuo hivyo inasemekana wengine tayari wanafanya shughuli zao binafsi na kujiajiri wenyewe huku wengine wakiwa wameajiriwa sehemu nyingine huku wakiendelea kupokea mishahara yao kama kawaida,” alisisitiza.

Alisema ameamua kuunda kamati hiyo baada ya kubainika kuwa watumishi wengi wa umma wameondoka mkoani Rukwa na kwenda masomoni kwenye vyuo vya elimu ya juu huku ikisemekana hawapo kwenye vyuo hivyo.

“Imebainika kuwa watumishi wengi wa umma wanapoajiriwa mkoani kwetu kiujanjaujanja tu wanaomba kwenda masomoni huku wakitumia majina tofauti ….tumeanza uhakiki kwenye vyuo vilivyopo mikoa ya jirani. Tumebaini kuwa wapo waliokwenda kusoma kusikojulikana na kusomea masomo tofauti huku wakiendelea kupokea mishahara,” alisema.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top