Maeneo mengine yatakayofanyiwa kazi ili kuboreshwa ni Sheria ya Mitandao, Sheria ya Kupata Taarifa, lakini pia kupelekwa bungeni kwa Muswada wa Sheria ili kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kupata huduma za kisheria.
Hayo yalisemwa juzi usiku na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe wakati akizungumza katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha TBC1, kwa lengo la kuainisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Katiba Mpya Inayopendekezwa
Akizungumzia Katiba Mpya Inayopendekezwa, Mwakyembea alisema mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania, ambao uliachwa kiporo na Serikali ya Awamu ya Nne, upo pale pale ingawa utekelezaji wake utakwenda polepole.
Alisema uthibitisho kuwa mchakato huo, utaendelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kauli iliyotolewa na Rais John Magufuli mara kadhaa kwamba serikali yake itaendelea na mchakato huo ili kupata Katiba mpya.
“Na mimi (Mwakyembe) niseme vivyo hivyo, nina uhakika kuwa litafanyika hivyo, alichokifanya Rais ni kuzipa nguvu mamlaka husika ili kuendelea na mchakato huo bila kuingiliwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Aliwataka wananchi kuendelea kuiamini serikali wakati ikiendelea na mchakato huo na kuongeza; “Tunayo Katiba ambayo tunaendelea kuitumia ili kuongoza nchi, hivyo tutaenda polepole na kazi hiyo ili kuhakikisha kuwa tutakapoimaliza tunapata Katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi walio wengi,” alisema.
Rushwa kwa mahakimu na majaji
Dk Mwakyembe alisema yamekuwepo malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu mfumo wa utoaji haki, huku wakiwanyooshea vidole Majaji na Mahakimu kuhusika na vitendo vya rushwa, hatua ambayo imeifanya serikali kuchukua hatua.
Alisema katika kupambana na tatizo la rushwa kwa Majaji na Mahakimu, serikali imeagiza kila wilaya na mkoa kuunda Kamati ya Maadili ya Mahakama ili ziweze kupokea masuala yanayohusu ukiukaji wa maadili kwa watendaji wa Mahakama.
“Mahakama ni chombo cha haki, ni lazima kiwe kitakatifu pasipo kutiliwa shaka, kuna sheria inayoagiza kila wilaya au mkoa kuwe na Kamati za Maadili ya Mahakama zenye kuangalia mwenendo wa Mahakimu kuanzia Mahakama za Mwanzo,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kamati hizo zitawasaidia wananchi wenye malalamiko kutoa madukuduku yao ambapo kwa ngazi ya wilaya, kamati hiyo inasimamiwa na Mkuu wa Wilaya na kwa Mkoa inasimamiwa na Mkuu wa Mkoa.
Waziri huyo alisema chini ya mkakati uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, malalamiko ya rushwa kwa Majaji na Mahakimu yatafika mwisho na kuongeza kuwa uundwaji wa kamati hizo ni hatua ya awali.
Divisheni ya Mahakama ya Rushwa
Kuhusu Divisheni ya Mahakama ya Rushwa, Waziri Mwakyembe alisema tayari Majaji 15 wamepelekwa Chuo cha Mahakama Lushoto kwa ajili ya kuongeza ujuzi na kuongeza uelewa wa namna ya kuendesha kesi za mahakama hiyo kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi tafsiri za sheria mbalimbali.
Alisema lengo la kuundwa kwa mahakama hiyo muhimu nchini ni kuongeza ufanisi katika kusikiliza kesi za rushwa na ufisadi wa aina mbalimbali.
“Kwa sasa tunamalizia maandalizi, vifaa na majengo tayari, pia majaji 15 wamepelekwa Lushoto ili waangalie maeneo yanayowashika wengi pamoja na kutafsiri sheria mbalimbali, yote hayo ni katika kujiandaa ili tusikwame,” alisema.
Alisema katika mahakama hiyo hakutakuwa na kesi za miaka iliyopita na kwamba kesi zitakazokuwa zikiwasilishwa huko zitakuwa zinasikilizwa na kuisha huku akisema sheria ya uanzishwaji wake ilianza kutumika rasmi Julai 8, mwaka huu, ikiwa imeainisha vigezo vya kesi zenye sifa za kutua katika mahakama hiyo.
Huduma ya kisheria kwa wasio na uwezo Kuhusu eneo hilo la huduma ya kisheria kwa wasio na uwezo, Waziri Mwakyembe alisema serikali itapeleka bungeni muswada wenye lengo la kuanzishwa kwa huduma hiyo lengo, likiwa ni kupanua wigo wa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia waweze kufikiwa.
Alisema, wizara yake tayari imeanza mchakato wa kuunda muswada huo wa kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria, ambayo itapelekwa bungeni hivi karibuni. Alisema hadi sasa kuna vikundi na asasi 290 zinazotoa huduma za kisheria nchini zikiwa na watumishi 4,500 na kwamba lengo ni kupanua zaidi wigo wa wananchi kuweza kupata huduma za kisheria hata kama hawana uwezo.
“Wanawake sasa wapige vigelegele, kwani majadiliano yataanzishwa ili kufikia maridhiano kwa wote kwani hii ni sheria inayogusa maslahi ya watu mbalimbali katika eneo la kimila, kidini na kiutamaduni.”
Alisema wanawake wamekuwa wakiteseka na kuonewa katika suala la mirathi na kwamba mara nyingi huonewa kwa sababu ya kukosa elimu.
Alisema serikali pia itapeleka bungeni muswada wa kutaka maridhiano kuhusu Sheria ya Ndoa na Mirathi ili wanawake wengi waweze kunufaika katika masuala ya mirathi tofauti na ilivyo sasa.
Kuhusu Sheria ya Mtandao alisema pamoja na kuwa hivi sasa sheria hiyo inatumika, lakini kumekuwepo na msuguano wa kimantiki baina ya pande mbili za wananchi, wakiwemo wanaosema inabana na wengine wakisema inalegezwa, hivyo serikali kuona umuhimu wa kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kuona suala hilo lipatiwe ufumbuzi bora zaidi.
Sheria ya Ndoa
Akizungumzia Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, Waziri Mwakyembe alisema rufani iliyokatwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu pingamizi la sheria hiyo, ina nia njema kwani inataka maridhiano yafikiwe kwanza na wananchi wenyewe kuhusiana na uboreshaji wa sheria hiyo badala ya kutumia njia ya mkato.
Alisema uamuzi wa Mahakama Kuu uliitaka Serikali kufuta vifungu viwili cha 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 vinavyoeleza mtoto wa miaka 14 na 15 anaweza kuolewa kwa idhini ya mzazi au Mahakama.
Alisema, serikali inaelewa, pia kilichosemwa na Mahakama si kigeni kwa serikali, na suala hilo pia lilifika katika Baraza la Mawaziri likajadiliwa kwa kina ikielezwa njia ya kutumia katika kupitisha sheria bila ya kutoka nje ya utamaduni wa maridhiano.
“Tanzania ina utamaduni wake wa maridhiano na kuongea, sasa muda umefika, kama serikali hakuna pingamizi lakini tutafikaje huko ni kwa nji ya ya mkato au kwa kuzungumza,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa ndio maana rufaa ilikatwa.
Kuhusu suala la umri wa mtoto wa kike kuolewa, Waziri huyo alisema serikali imeliona, lakini ingependa Watanzania kujadiliana kwanza, na kwamba isitafsiriwe kuwa serikali inapinga maoni ya wadau bali inachokifanya ni kuangalia njia bora zaidi ya kufikia azma hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )