'Kwenye swala la mapenzi wanaume hawana mzaha'
Katika
Gazeti la Mwananchi la hivi karibuni la May 18, 2010, kuna habari
iliyoandikwa na mwandishi Anthony Kayanda wa Kigoma ambayo
ilinisikitisha sana. Habari yenyewe ni ile iliyohusu mtu mmoja kuuwawa
kwa kuchomwa kisu kifuani kwa tuhuma za kutembea na mke wa mtu.Kwa
mujibu wa Gazeti hilo, tukio hilo limetokea katika kijiji cha Kitagata
kilichopo katika tarafa ya Makere, Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.
Marehemu
ametajwa kuwa ni Ally Bwisigwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.Ilidaiwa
kwamba Marehemu alikuwa akitembea na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa
jina moja la Perusi ambaye aliwahi kuolewa na Hassan Rashid mkazi wa
Kasulu Mjini na waliishi pamoja kwa muda mrefu kabla ya mume huyo
kufungwa gerezani.Baada ya mumewe kufungwa, Perusi alirudi kijijini kwao
huko Kitagata na ndipo alipoanza mahusiano ya kimapenzi na marehemu.
Inadaiwa
kuwa baada ya Mume huyo kutoka Gerezani alimuonya mtuhumiwa mara kadhaa
kuacha kutembea na mkewe lakini marehemu aliendelea na mchezo wake huo
mchafu.Inadaiwa kuwa Hassan alifanya majaribio mawili ya kutaka kumuua
marehemu kwanza kwa kutaka kumgonga na pikipiki na tukio la pili
lilikuwa ni lile la kumchoma kisu ambapo hata hivyo kisu hicho
hakikumpata.
Nimesema
kuwa tukio hilo limenisikitisha sana kwa sababu bado nashindwa kuelewa
hivi inakuwaje mpaka mtu unapoteza maisha kwa sababu ya mwanamke, tena
kibaya zaidi mke wa mtu!Ingawa inasemwa kwamba wanawake ni viumbe wa
ajabu lakini naamini wanaume ndio viumbe wa ajabu kupindukia.
Kwa
nini ninasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu, wanawake kwa ujumla wao
wanavyo vibweka vyao katika swala zima la mapenzi, lakini ukija kwa
wanaume naamini nao wanavyo vibwekwa vyao tena vya hatari ukilinganisha
na vile vya wanawake.Kwa mfano, hivi ni mara ngapi tumeshawahi kusikia
baadhi ya wanaume wakiamua kujinyonga kwa sababu ya kushindwa
kuwashawishi wanawake wanaowapenda?
Namini
kuwa matukio ya aina hiyo yapo sana na sio kwa huko nyumbani tu bali
pia hata katika nchi zilizoendelea. Linapokuja swala la mapenzi kuna
baadhi ya wanaume wanakuwa kama Nyati waliojeruhiwa, na ndio sababu
unaweza kukuta baadhi ya wanaume wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama
vile vya wizi au ujambazi kwa lengo la kuwashawishi wanawake
wanaowapenda ili wawakubali. Wakati mwingine hujiingiza kwenye matumizi
ya Pombe kupita kiasi au hata matumizi ya Bangi na madawa ya kulevya
kutokana na kuachwa na wanawake wanaowapenda.
Tabia
hii ya wanaume kuhatarisha maisha au hata kupoteza maisha kama
tulivyoona katika tukio hilo la Kigoma ni la tangu enzi za kale. Kuna
simulizi nyingi tulikuwa tukisimuliwa enzi za utoto wangu huko nyumbani
kwamba kuna wakati wanaume walikuwa wakipigana ili kumgombea mwanamke na
shujaa anayeshinda katika ugomvi ndiye anayemchukuwa mwanamke
anayegombewa.
Inaonekana
wazi kwamba uwezekano wa mwanaume kufa mapema au kuhatarisha maisha
yake ni mkubwa ukilinganisha na ule wa wanawake. Na hiyo inatokana na
wanaume kupenda sifa na kutaka kuwamiliki wanawake wawapendeo. Kuna
matukio mengi ya kusikitisha ambayo huwa tunayasoma katika vyombo vyetu
vya habari ambapo matukio kama yale ya mwanaume kumuua mwanaume mwenzie ili kumpata mwanamke ampendae ni vya kawaida kabisa.
Kwa
mfano katika tukio hilo la Kigoma, licha na kukoswa koswa kuuwawa mara
mbili lakini marehemu hakukoma kutembea na mke wa mwenzie, mpaka
akasababisha kupoteza maisha.Hivi kumekuwa na uhaba wa wanawake kiasi
cha kupelekea baadhi ya wanaume kuhatarisha maisha yao au kupoteza
maisha kutokana na kumgombea huyu kiumbe mwanamke au kuna kitu kingine
kinachotafutwa hapo?
Ni
aghalabu sana kusikia mwanamke kamuua mume baada ya kumfumania au
kumuua mgoni wake tofauti na wanaume. Kama ukipima jambo hilo kitakwimu
basi utapata idadi ya wanaume ya kutosha ukilinganisha na ile ya
wanawake.
Kimsingi
wanaume wamewageuza wanawake kama mali zao wanazozimiliki na hiyo ndio
sababu inapotokea kumfumania mkewe au mchumba wake akiwa na mwanaume
mwingine mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza atamuadhibu mgoni wake au
hata kumuua kisha mke naye atasulubiwa au hata kuuawa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )