Waziri wa Elimu, Prof Joyce Ndalichako
Wawanafunzi
wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele Mkoa wa
Katavi, wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko walimu wao wawili
miongoni mwao akiwemo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Makonda Ng’oka
“Membele'‘ (34) ambaye ameng’olewa meno matano kwa kipigo hicho.
Walimu
hao wawili wamedai kuwa hawako tayari kuendelea kufundisha katika shule
hiyo huku wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa viboko na
wanafunzi wao wenyewe ambapo Mwalimu Gabriel Kambona aliachwa na ngeu
kichwani.
Mei
mwaka huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa
Katavi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda kosa
hilo kati ya Novemba 2015 na Aprili mwaka huu.
Ilisemekana
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo
kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano sasa wako Kidato
cha Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga
vitendo vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.
Wanafunzi
hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni
adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.
Hata
hivyo, baada ya kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani Ng’oka, Julai
27, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda ilimwachia
huru.
Mwalimu
Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha kazi shuleni Usevya Agosti Mosi
mwaka huu ambako kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa kuamsha hasira
kwa baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wakidai hawapo tayari kumwona
mwalimu huyo na familia yake shuleni hapo.
Akizungumza
na wanahabari jana mjini hapa, Ng’oka alidai kuwa hayuko tayari
kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama wake na kutokana
na kipigo alichokipata cha kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa
kidato cha tano na cha sita wakati akiwa nyumbani kwake na familia yake.
Akisimulia
mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka huu usiku alikuwa nyumbani kwake
shuleni hapo pamoja na familia yake pamoja na mwalimu mwenzake, Gabriel
Kambona aliyekuwa amemtembelea.
“Ghafla,
saa mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga lilitokea kundi la wanafunzi
wa kidato cha tano na sita wakiwa na silaha za jadi kama vile fimbo,
marungu, mawe na matofali na kuanza kuishambulia familia yangu pamoja na
mwalimu Kambona,” alieleza na kuongeza kuwa alilazimika ‘kuchomoka’
bafuni baada ya kusikia mayowe yaliyokuwa yakipigwa na familia yake
wakiomba msaada. Alipofika sebuleni alishuhudia wanafunzi hao
wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza viboko.
“Ndipo
walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa marungu na fimbo
hadi nikapoteza fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye Kituo cha
Afya Usevya na kubaini kuwa nimepoteza meno yangu matano huku nikiwa
nimejeruhiwa vibaya kichwani. Baadaye nilihamishiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa wiki moja na nusu kwa matibabu na sasa
nimepewa rufaa niende Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar kwa
matibabu zaidi,” alieleza.
Alidai
kuwa uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda mrefu, lakini
anashangaa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele
umeshindwa kumpangia kituo kingine cha kazi na kuchukua hatua yoyote kwa
wanafunzi hao licha ya kupeleka majina yao kwa kuwa anawafahamu wote
waliohusika.
Mwalimu
Kambona alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule
hiyo kwamba kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake kimemfedhehesha.
Kwa
mujibu wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo waliketi baada ya kutokea
kwa tukio hilo, na walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote waliobainika
kushiriki kuwashambulia walimu wao wasimamishwe shule akidai kuwa
uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele ulipinga.
“Nimeandika
barua ya kuomba uhamisho kwani nia aibu kwangu kuendelea kufundisha
wanafunzi ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani ….. siku hiyo
ya tukio niliibiwa simu mbili za kiganjani lakini jana nimefanikiwa
kuikamata simu moja kwa mwanafunzi wa kidato cha tano anayeitwa , Alex
Maiko Makona na tayari amemfikisha katika Kituo cha Polisi cha Usevya,” alidai.
Mwenyekiti
wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Katavi, Gregori Mshota alisema tayari
chama chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe
na uongozi wa Wilaya ya Mlele ili kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa
salama.
Ofisa
Elimu wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju alidai kuwa suala hilo lipo
ofisini kwake na wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili linahitaji
ushirikishwaji wa vyombo mbalimbali ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari
ya Usevya,” alieleza.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara mkoani Katavi mwezi
uliopita, mke wa mwalimu Ng’oka alitinga kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kijijini Maji Moto akiwa na bango lenye malalamiko ya
kutishiwa usalama wa maisha wa familia yake, na Waziri Mkuu alimwagiza
Kamanda wa Polisi wa Mkoa kushughulikia malalamiko hayo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )