UONGOZI wa Simba umesema unafanya mpango wa kumrejesha kikosini
mshambuliaji wake wa zamani Emmanuel Okwi aliyevunja mkataba na klabu ya
Sonderjyske ya Denmark.
Taarifa za kwenye mtandao wa klabu hiyo juzi ziliandika kwamba Okwi
amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kukosa nafasi ya
kucheza kwenye kikosi hicho.
Jana jioni Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliandika kwenye kurasa
zake za mitandao ya kijamii: “Kocha Omog (Joseph- kocha mkuu wa Simba)
ikimpendeza, Emmanuel Okwinho (Okwi) dimbani Feb 18, hiyo ndio habari
mpasuko, ukinuna ongeza limao,”.
Simba inatarajia kucheza na Yanga katika mechi ya raundi ya pili ya
Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Manara alikiri kuwa
uongozi wake uko kwenye mchakato wa kumnasa mchezaji huyo na ikiwezekana
atumike kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu.
“Ni kweli tutamsajili kama mchezaji huru,” alisema.
Hata hivyo, tayari dirisha dogo la usajili kwa klabu za ligi
limeshafungwa mpaka msimu ujao. Akilizungumzia hilo, ofisa habari wa
Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema Simba haiwezi
kumtumia Okwi kwa sababu dirisha la usajili limeshafungwa.
“Ingewezekana kama usajili wa dirisha dogo ungekuwa haujafungwa,
lakini dirisha limeshafungwa hivyo kama wanataka kumtumia, wasubiri
mpaka usajili mwingine,” alisema.
Wakati wa usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana Simba ilitaka
kumsajili mshambuliaji huyo Mganda lakini ilishindwa baada ya klabu ya
Sonderjyske kutaka ilipwe karibu sh milioni 240.
Hasimu wa Simba, Yanga pia ilijaribu kutaka kusajili mshambuliaji
mwingine ili ashindane na Donald Ngoma baada ya kudaiwa kugoma kucheza
kwenye mechi za kombe la Mapinduzi lakini ilishindikana kwa vile dirisha
la usajili lilishafungwa.
Sonderjyske ilimsajili Okwi Julai 2015 kutoka Simba kwa mkataba wa
miaka mitano uliotakiwa kumalizika mwaka 2020 ambapo tangu amesajiliwa
Okwi alicheza mechi nne tu za Ligi Kuu ya Denmark na mbili za kombe la
DBU ambapo alifunga mabao mawili.
Simba pia iliwahi kumuuza Okwi Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013
kwa dola za Marekani 300,000 kabla ya kusajiliwa na Yanga alipocheza kwa
muda mfupi na kurejea Simba.
Okwi ni mshambuliaji kipenzi cha wanasimba kutokana na mafanikio
aliyoipatia timu hiyo ambapo jana baada ya Manara kuweka suala lake
kwenye mitandao ya kijamii, karibu mashabiki wengi wa soka walikuwa
wakimzungumzia.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )