Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi kufuatia vifo vya watu 12 vilivyosababishwa na ajali ya magari
mawili kugongana uso kwa uso.
Ajali
hiyo imetokea tarehe 23 Novemba, 2017 majira ya saa 2:30 usiku katika
eneo la Ighuka Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida ambapo basi dogo aina ya
Toyota Hiace lililokuwa limebeba watu waliotoka kwenye sherehe ya
harusi limegongana na gari dogo aina ya Noah lililokuwa linatoka
msibani.
Katika
salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rehema Nchimbi kufikisha
salamu zake za pole kwa familia zilizopoteza jamaa zao, ndugu na
marafiki.
“Ajali
hii imeleta majonzi makubwa sio tu kwa familia zilizopoteza jamaa zao
bali kwetu sote, tumepoteza ndugu zetu wengi ambao wameacha familia zao,
wapendwa wao na jamaa waliowategemea, kwa hakika hili ni pigo kubwa”
“Naungana
na familia za Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na pia
nawaombea Marehemu wapumzike mahali pema, wote walioguswa na vifo hivi
wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amevitaka vyombo vinavyosimamia matumizi ya barabara
na usalama barabarani, kuongeza juhudi katika udhibiti wa ajali na
kuwachukulia hatua kali wote wanaovunja sheria na kusababisha ajali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Novemba, 2017
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )