Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema hakuna waziri mwenye ubavu wa kukataa akimtuma jambo.
Amesema
hayo jana Ijumaa Novemba 24,2017 katika mkutano wa hadhara uliofanyika
Kijiji cha Moita Bwawani akimnadi mgombea wa CCM wa Kata ya Moita wilaya
ya Monduli, Prosper Damuni.
"CCM
ndiyo chama kilichoshika dola kama kuna changamoto sehemu yoyote
namwambia waziri anayehusika anafika haraka eneo hilo kusikiliza na
kutatua changamoto hiyo, hakuna waziri mwenye ubavu wa kukataa
nikimtuma," alisema Kinana.
Katibu
mkuu huyo amewaomba wananchi katika kata 43 zinazofanya uchaguzi mdogo
wa udiwani kuwachagua wagombea wa CCM akisema ndicho chama kinachoongoza
dola na ahadi zinazotolewa zinatekelezeka.
Kinana amewaomba wananchi hao akisema ni wakati muafaka kwao kuacha kupiga kura kwa ushabiki.
Alisema
wilaya hiyo inakusanya mapato ya ndani ya Sh2 bilioni kwa mwaka wakati
bajeti yao kwa mwaka ni Sh49 bilioni kwa mwaka fedha ambazo zinatolewa
na Serikali Kuu hivyo ni muhimu kuwa na diwani anayetoka chama hicho ili
kurahisisha maendeleo ya wananchi.
Kinana alisema anafahamu wilaya hiyo ina changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kutatuliwa.
"Nataka
nimpe mbinu mgombea wenu akichaguliwa anatakiwa kuwa karibu sana na
mkurugenzi mtendaji wa wilaya na kwa kuwa anatokana na CCM atakuwa na
uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ofisi za Serikali kutafuta fedha za
maji, barabara, afya na elimu hiyo ndiyo kazi ya diwani si kukaa tu
kusubiri maendeleo yaje," alisema Kinana
Katika
mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa mikoa, Mrisho Gambo wa Arusha na
Christopher ole Sendeka wa Njombe waliwataka wananchi kutoyumbishwa na
kelele za vyama vingine bali wamchague mgombea wa CCM.
Mgombea
udiwani, Damuni aliwaomba wananchi kumchagua ili alete maendeleo kwa
kuzingatia chama chake ndicho kinachotekeleza ilani ya uchaguzi
iliyoshinda mwaka 2015 na kuunda Serikali.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )