Polisi
Mkoa wa Kilimanjaro wamelazimika kutumia mabomu ya machozi ili
kuwatawanya wananchi kumwezesha mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kupata nafasi ya kupita mjini
Moshi.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walitumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wamefunga barabara.
Takriban
mabomu manne ya kutoa machozi yalifyatuliwa saa 10:30 jana jioni ya
Jumamosi Novemba 18,2017 katika eneo la Soko la Manyema ambako Lowassa
na msafara wake alikuwa apokewe ili kuelekea kwenye mkutano wa hadhara
wa kampeni za udiwani eneo la Pasua Relini.
Kabla ya Lowassa kufika, vijana madereva wa bodaboda walipita katika Barabara ya J.K. Nyerere.
Vijana
hao walipopita mzunguko wa magari wa Coca Cola saa 10:15 jioni, gari la
polisi aina ya Toyota Land Cruicer likiwa na polisi wenye mabomu ya
machozi lilionekana likiwafuata.
Haikupita dakika 15, ndipo kulisikika milio ya mabomu katika eneo la Manyema ambalo ni njia panda ya kuelekea eneo la mkutano.
Katibu
wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema ambaye yuko katika msafara
wa Lowassa, alisema eneo la Manyema lilikuwa halipitiki kutokana umati
wa watu.
Lema
alisema ni kutokana na hali hiyo, ili kumwezesha Lowassa na msafara
wake kupita, FFU walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mabomu hayo
yamepigwa ili kupunguza idadi ya watu waliokuwa wamefurika kwenye eneo
hilo na kumuwezesha Lowassa kupita.
“Alikuwa
hana njia ya kupita, watu walifurika kiasi kwamba hata Lowassa mwenyewe
asingeweza kupita, tulifanya hivyo kuwapunguza na ameshapita ameenda
zake kwenye mkutano,” alisema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )