Bunge
la Afrika Mashariki (Eala) limemchagua Spika kutoka Rwanda, Dk Martin
Ngoga katika uchaguzi ulioibua mabishano ya kisheria juu ya uhalali wa
kufanyika kwake.
Baada
ya dua ya kuliombea Bunge, mbunge Dk Ngwaru Maghembe kutoka Tanzania
aliomba mwongozo wa kuliahirisha kutokana na akidi kutotimia kutokana na
wabunge tisa wa Burundi na saba wa Tanzania kutokuwepo kwa sababu
ambazo hazikujulikana.
Mbunge
kutoka Uganda, Freddy Mbidde alipinga hoja hiyo akisema kanuni ya 53(1)
inayozungumzia akidi inahusu Bunge rasmi ambalo tayari lina Spika
lakini kwa kuwa hawakuwa na Spika kanuni hiyo haina nguvu kisheria.
Mbunge
mwingine wa Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema kutokana na Bunge
kuchelewa kuanza kazi kwa kipindi cha miezi sita kutokana na mwanachama
wa EAC nchi ya Kenya kuchelewa kuchagua wabunge ni busara uchaguzi
usifanyike hadi wabunge wote wawepo.
Hoja
hiyo ilipingwa na mbunge kutoka Uganda, Suzane Nakauki aliyedai hoja ya
kutokufanya uchaguzi kwa sababu ya wabunge kutokuwepo haina mashiko
kisheria na kikanuni kwa sababu wameorodhesha majina yao kwenye kitabu
cha mahudhurio na wamepewa posho na wameamua kwa sababu zisizojulikana
kugomea uchaguzi.
Alisema
haiwezekani wabunge wa Tanzania ambao wapo nchi mwao washindwe
kuhudhuria kikao cha Bunge wakati wapo jijini Arusha, huku waliotoka
mbali wakiwepo.
Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Liberat Mfumukeko
alisema kila jambo lenye mgogoro kwenye mihimili ya EAC lina utaratibu
wa kulimaliza kwa njia ya kuomba ushauri kwa sekretariati, Mahakama,
baraza la mawaziri na kikao cha marais.
Hatua
hiyo ilimwinua Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Isabella Ndahayo
aliyesema wabunge wa Burundi hawakuridhishwa na utaratibu wa uchaguzi
licha ya kanuni kutamka wazi nafasi ya Spika ni ya mzunguko kwa nchi
wanachama.
"Wabunge
wa Burundi hawapo kwa sababu hawaridhiki na kinachoendelea, naomba
tupewe tafsiri ya nafasi ya Spika kuwa ni mzunguko kwa nchi wanachama,
si kwamba tunapinga juhudi za mshikamano wa jumuiya bali tafsiri
halisi," alisema Isabella.
Naibu
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda ambayo ni
Mwenyekiti wa EAC, Julius Wandera alisema kumekuwa na mashauriano kati
ya baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo ili kuhakikisha suala hilo
linakamilika.
Baada
ya mabishano ya kisheria na kanuni, katibu wa bunge aliamua uchaguzi
kufanyika na awamu ya kwanza, mgombea kutoka Rwanda, Dk Martin Ngoga
alipata kura 35, Leontine Nzeyimana wa Burundi kura moja na Adam Kimbisa
wa Tanzania hakupata kura.
Kutokana
na kanuni kuhitaji mshindi kupata theluthi mbili ya kura zote 52,
uchaguzi ulirudiwa kwa kanuni ya mshindi kupatikana kwa wingi wa kura na
Dk Ngoga aliibuka mshindi kwa kupata kura 33 dhidi kura tatu za
Nzeyimana ambaye hakuwepo bungeni.
Baada
ya kula kiapo Dk Ngoga ambaye alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa Rwanda
alisema anafahamu uchaguzi wowote lazima uache majeraha lakini yupo
tayari kushirikiana na kila mbunge kujenga jumuiya hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )