Aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake
watano jana Jumatano walipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo
kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na
kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.
Kabla
ya kusomewa mashtaka ya kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi namba 80 ya
2017, mahakama ilimfutia kesi iliyokuwa na mashtaka matano yanayofanana
na hiyo iliyofunguliwa mwaka 2014.
Kesi
hiyo ilifutwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa baada ya
Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuomba iondolewe kwa kuwa Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Kesi
hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa
upande wa mashtaka na mashadi tisa walikuwa wamekwishatoa ushahidi wao
na washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana.
Baada
ya kesi hiyo kufutwa, Madabida ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa kiwanda
hicho na wenzake walikamatwa tena na kufunguliwa kesi hiyo mpya ya
uhujumu uchumi.
Mbali
na Madabida wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Seif Shamte ambaye ni
mkurugenzi wa uendeshaji, Simon Msoffe (meneja masoko) na Fatma
Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd.
Pamoja na Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu
ya Dawa.
Baada
ya kusomewa mashtaka washtakiwa hao hawakurusiwa kuongea chochote kwa
sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi
hiyo hadi Mahakama Kuu.
Wakili
wa Serikali, Pius Hilla alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika
lakini DPP bado hajafanya maamuzi kama isikilizwe Kisutu ama Mahakama
Kuu.
Washtakiwa hao wanatetewa na Mawakili Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemiah Nkoko.
Wakili
Msafiri alisema Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuisikiliza hiyo
kwa sababu kiwango chake cha fedha kipo chini ya Sh 1 bilioni ambayo
ndiyo inapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu.
Kutokana na hoja hiyo Wakili Hilla aliomba wapewe muda hadi leo Alhamisi ndiyo wajibu hoja ya upande wa utetezi.
Hakimu
Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi leo Alhamisi kutokana na ombi hilo
na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi leo Alhamisi
itakaposikilizwa hoja kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kuisikiliza kesi
hiyo ama la.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )