Siku
chache baada ya Rais John Magufuli kubainisha kukamatwa kwa kiasi
kikubwa cha fedha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere
(JNIA) aliyekamatwa na fedha hizo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu.
Mshtakiwa huyo ni Raia wa Uganda, ambaye ni Kalani wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA, Winfred Businge (33).
Busige
amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la kushindwa kuelezea kwa
mamlaka ya forodha fedha alizokamatwa nazo Airpot ambazo ni USD Milioni
moja(takribani Sh.Bil 2).
Wakili wa serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja.
Amedai kuwa kosa hilo amelitenda kinyume na kanuni za sheria za utakatishaji fedha, ambayo haimnyimi mshtakiwa dhamana.
Wakili
Mbagwa amedai kuwa Businge ametenda kosa hilo December 11, 2017 katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Inadaiwa
akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alikutwa ameingia nchini akiwa na
USD Milioni 1 (zaidi ya Sh.Bil 2) ambazo alishindwa kuzitolea maelezo
kwa wakala wa forodha.
Baada
ya kusomewa kosa hilo, mshtakiwa alikana kosa, ambapo wakili Mbagwa
alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa
ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Emmanuel Safari alimuombea dhamana mteja wake.
Hakimu Shaidi alimuachia mshtakiwa huyo kwa masharti ya dhamana ya mdhamini mmoja bila kusaini bondi.
Hakimu
Shaidi amesema amemuachia kwa dhamana bila bondi kwa sababu fedha
zilizokamatwa zitakuwa kama dhamana yake. Kesi imeahirishwa hadi January
18,2018.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )