Spika
wa Bunge, Job Ndugai amepinga mpango wa Serikali wa kuwapangia vituo
vya kazi moja kwa moja walimu wanaoajiriwa, akihoji ni kwa nini inapoka
madaraka ya halmashauri.
Ndugai
ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 23,2017 ikiwa ni siku moja baada
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo kutangaza majina
ya walimu 3,033 waliopangiwa vituo vya kazi.
Katika
kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Dodoma leo, Spika Ndugai amehoji
Tamisemi ni nani hata aweze kujua ikama ya walimu shuleni. Amesema
wamekuwa wakijaza walimu maeneo yasiyo na mahitaji.
"Hili
jambo linakera, yaani kila mahali sasa ni Tamisemi hadi napata shaka
sasa, hivi hii zana ya D by D (ugatuaji wa madaraka) ina maana
haijatafsiriwa vyema au ndiyo kupoka madaraka kwa wengine," alihoji
Ndugai.
Spika
ametoa mfano wa Shule ya Banyibanyi wilayani Kongwa ambayo amesema ina
wanafunzi wanaoingia kidato cha tatu lakini hawajawahi kusoma masomo ya
sayansi hata siku moja.
"Lakini
juzi hapa mmepanga walimu na nilipita tena hapo hakuna hata mwalimu.
Hawajasoma hesabu, fizikia, baiolojia, kemia na jiografia; nauliza tena
wanasema Tamisemi, hivi hao walisoma wapi na ninyi mmesoma shule zipi,"
alihoji.
Ndugai
amewatupia mzigo wabunge wa Mkoa wa Dodoma amesema wanatakiwa kuupinga
mpango huo bungeni wakati yeye akiongoza vikao vya Bunge.
Pia, amepinga mpango wa utoaji fedha kwa vikundi amesema umepitwa na wakati kwa kuwa zinaliwa bure.
Amesema
hakuna umuhimu wa kusema watu waunde vikundi ndipo wapewe fedha au
uwezeshwaji, badala yake waangaliwe mtu mmoja mmoja ambao wanakuwa na
uwezo wa kuzalisha na kisha wafuatiliwe.
Mbunge
wa Mtera, Livingstone Lusinde na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Profesa
Davis Mwamfupe kwa nyakati tofauti waliunga mkono hoja ya kutopeleka
fedha kwa vikundi.
Lusinde amesema kumekuwa na utitiri wa vikundi baada ya kusikia kuna fedha wakati uwezo wa uzalishaji haupo.
"Namuunga
mkono Spika katika hili, tunaunganisha watu hata wasiokuwa na mbinu za
uzalishaji, naomba tuachane na vikundi havina tija kwa kuwa wanagawana
fedha tu," amesema Lusinde.
Profesa
Mwamfupe amesema Serikali inagawa vibaya rasilimali fedha kwa kauli ya
kasungura kadogo tugawane lakini zinaishia kutoleta tija.
Akijibu
hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewaagiza
wakurugenzi wa wilaya kuangalia ikama ya walimu na kuwatawanya mara
moja.
Kuhusu
fedha za vikundi kwa vijana na akina mama amesema jambo hilo liko
kisheria. Amesema hakuna ubaya kuwasaidia watu mmoja mmoja ambao
wanajiweza katika uzalishaji.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )