Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye jina lake linatajwa kutaka kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, anaelezwa kutamani kuingia katika hatua za mwisho za kinyang’anyiro hicho na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Vyanzo
vya habari ndani CCM vinasema kwamba Membe amekua akionyesha kutamani
kuingia katika hatua ya 'tatu bora' pamoja na Lowassa ili aonyeshe uwezo
wake ndani ya chama hicho, tofauti na wapinzani wake wanaodai hana
nguvu kisiasa na hawezi kushindana na Lowassa ndani ya chama.
"Membe
anatamani sana kama akigombea aingie na Lowassa katika hatua ya mwisho
maana anatamani aonyeshe uwezo wake, kama alivyowaonyesha katika
uchaguzi wa kuingia NEC (Halmashauri Kuu ya CCM) mwaka 2012, ambao
walimpiga vita na kutumia fedha nyingi lakini akapata kura za kutosha
bila kampeni ya nguvu na kuwatia aibu," anasema mtoa habari huyo ndani ya CCM.
Katika
uchaguzi huo wa mwaka 2012 ambao Lowassa hakugombea katika ngazi ya
Taifa na badala yake aligombea kupitia Wilaya ya Monduli, Membe alipata
kura 1,455 ikiwa ni asilimia 74 ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM pamoja
na kupigwa vita na wanasiasa ili asipite na kuingia NEC.
Hata
hivyo, habari za ndani ya CCM zinaeleza kwamba kupita kwa Lowassa ni
mtihani mgumu kwa chama hicho kutokana na ukiukwaji wa maadili anaodaiwa
kuufanya mwanasiasa huyo ambaye ni Mbunge wa Monduli.
Baadhi
ya ukiukwaji wa maadili anaodaiwa kuufanya Lowassa ni pamoja na kufanya
kampeni wakati akiwa katika adhabu anayotumikia na wenzake watano,
akiwamo Membe, ambao walifungiwa kwa miezi 12.
Wengine
katika orodha hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William
Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Kilimo na
Chakula, Steven Wasira.
Juhudi
za kumpata Lowassa kutoa maoni yake kuhusu matamanio hayo ya Membe
hazikufanikiwa kwa vile inaelezwa kwamba yuko mapumziko visiwani
Zanzibar ambako amepumzika na pililapilika za kisiasa.
Hata
hivyo, Msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo, alisema ingawa ingekuwa
vema zaidi kama bosi wake huyo angejibu mwenyewe kuhusu jambo hilo, kwa
sasa bado ni mapema kuzungumza kuhusu kinyang’anyiro hicho.
“Hili
si suala la kisera na limekaa kibinafsi na hivyo nadhani Mzee (Lowassa)
mwenyewe angeweza kuzungumza. Hata hivyo, akizungumza kuhusu hilo
inaweza kutafsiriwa kwamba anapiga kampeni na hivyo naona ni mapema kwa
sasa kusema lolote,” alisema.
Lakini
wakati msemaji huyo akibainisha hayo, tayari baadhi ya wanasiasa
walioko kwenye kambi hiyo ya Lowassa wamekuwa wakijigamba kuwa na nguvu
ndani ya chama hicho, hasa katika Halmashauri Kuu (NEC) na Mkutano Mkuu,
hali inayonogesha mpambano huo wa fainali ambao Membe anatajwa
kuutamani kama atatangaza kuwania na kisha kuteuliwa.
Hofu
ya kwamba Lowassa anaweza kukatwa jina lake na vikao vya CCM
inachangiwa na mambo mengine kadhaa anayotajwa kuyafanya kiasi cha
kukiuka masharti ya adhabu aliyopewa sambamba na makada wenzake hao
ndani ya CCM.
Miongoni
mwa matukio yaliyosababisha hadi Lowassa kuonywa na Sekretariati ya CCM
kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ni kuandaa makundi
kadhaa yaliyokuwa yakifika nyumbani kwake, Dodoma na Monduli (Arusha),
kwa ajili ya kile kilichokuwa kikielezwa ni kumwomba (kumshawishi)
agombee urais.
Tayari
kundi la Lowassa limekwishaweka bayana kwamba ‘ushawishi’ huo ni
mwitikio wa wito alioutoa Rais Jakaya Kikwete, Songea, mkoani Ruvuma
katika maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM kwamba wanaCCM
wajitokeze kushawishi wenzao wanaodhani wanafaa kuwania urais.
Pamoja
na utata huo unaozunguka suala la Lowassa, bado Membe amewaambia
wenzake kwamba endapo ataamua kugombea, angetamani kinyang’anyiro hicho
kimshirikishe Mbunge huyo wa Monduli ili “mzizi wa fitina” kuhusu suala
hilo la nani ana nguvu ndani ya CCM uweze kukatwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )