Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, jana lilishindwa kuendelea kumhoji Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu tuhuma za kumtukana
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Gwajima
alifika katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central), jana asubuhi,ikiwa ni
siku mbili tangu aliporuhusiwa kutoka katika Hospitali ya TMJ alikokuwa
amelazwa kwa matibabu.
Wakili wa askofu huyo, John Mallya alisema jana
kuwa mteja wake alifika kituoni hapo saa 2.10 asubuhi, lakini Msaidizi
wa Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam alipomuona, alisema hawawezi
kumhojiano kwa kuwa afya yake haijaimarika.
“Alitutaka turudi na
badala yake kufike kituoni hapo Aprili 9, mwaka huu,” alisema Wakili
Mallya aliyeongozana na Askofu Gwajima pamoja na wachungaji wanane wa
kanisa hilo.
Askofu Gwajima
alijisalimisha mwenyewe kituoni hapo Ijumaa iliyopita, baada ya
kutakiwa kufanya hivyo na Jeshi la Polisi, akituhumiwa kumkashfu
Kardinali Pengo wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, wakati
akiendesha ibada kanisani kwake.
Awali, wakati akihojiwa, aliishiwa nguvu na hatimaye kupoteza fahamu, hivyo kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Katika hatua
nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amesema Askofu
Gwajima lazima atahojiwa na ofisi yake ili kujiridhisha zaidi na
shughuli anazozifanya, ikiwamo umiliki na uhalali wa kutumia eneo la
Kiwanja cha Tanganyika Packers, kilichopo Kawe.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )