Zaidi ya madiwani 20 wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), jana walivamia ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam kumshinikiza Kaimu Mkurugenzi wake, Sarah Yohana kuitisha Baraza
la madiwani kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa meya na naibu wake.
Madiwani
hao waliovamia ofisi hiyo jana, walisema kikao hicho kinatakiwa
kuitishwa ndani ya siku saba kikiwa na ajenda moja ambayo ni uchaguzi wa
meya na naibu wake, ambao umekwama mara kadhaa kwa kile walichodai kuwa
ni hila na hujuma.
Uchaguzi huo umeahirishwa mara tatu kwa
sababu mbalimbali, Januari 23 uliahirishwa kutokana na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kutoa muda kwa mameya wa
manispaa zinazounda Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam; Kinondoni,
Temeke na Ilala kuandaa mfumo bora wa kuwapata wajumbe watatu
watakaounda Baraza la Jiji.
Februari 8, uliahirishwa kutokana na
kubainika kwa nyongeza ya majina 14 yaliyopenyezwa kutoka halmashauri
za Kinondoni na Ilala ambao hawakustahili kushiriki kikao hicho, pia
Februari 27 uliahirishwa kutokana na zuio feki la mahakama.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana baada ya kukaa zaidi ya saa tatu bila kuonana
na Yohana, madiwani hao na wabunge walisema wamechoshwa na uongozi wa
jiji kuwahadaa kama watoto wadogo.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee
alisema wamechoka kupigwa danadana na kwamba wanachohitaji ni uchaguzi
wa Meya wa Dar es Salaam kufanyika ndani ya siku saba siyo vinginevyo.
“Tumekaa
zaidi ya saa tatu wametwambia Yohana hayupo, sasa akija mfikishieni
taarifa kuwa Ukawa hatuna maelezo na Jumatatu tutatia timu tena hapa
ofisini kwake,” alisema Mdee akimpa maagizo Ofisa Utawala wa Dar es
Salaam, Iman Kasagara.
“Narudi tena, mfikishieni salamu,
Jumatatu hatutaki kusikia longolongo za aina yoyote kutoka kwake.
Tunataka majibu ya kueleweka vinginevyo hatutamuelewa,” alisema Mdee
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).
Kasagara aliahidi kufikisha ujumbe huo kwa mhusika ambaye ilidaiwa alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti
wa Madiwani wa Ukawa Dar es Salaam, Manase Mjema alisema uvumilivu
umewashinda kutokana na figufigisu zinazofanywa na Jiji la Dar es Salaam
kuhusu uchaguzi huo.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara
alisema ajenda kuu ya Ukawa ni uchaguzi wa meya na wameacha shughuli
zote hadi suala hilo lipatiwe ufumbuzi.
“Sasa hivi wakurugenzi
akiwamo wa Dar es Salaam, wamepeleka bajeti zao hazina bila kushirikiana
na meya kwa sababu hajapatikana, hivi hapo kuna maendeleo kweli?” alihoji Waitara.
“Kimsingi utaratibu wa kisheria ulishapita, sasa tunaelekea siku 90 bila meya tumechoka na hali hii,” alisema Waitara.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )