Tokea aapishwe kuwa rais wa awamu ya tano Tanzania, Novemba 5, mwaka jana, Rais Dk. John Pombe Magufuli amekuwa msiri katika uteuzi wake, kwani mara nyingi amekuwa akiibuka na watu wasiotarajiwa, kitu kinachowapa hofu viongozi waliopo madarakani hivi sasa, kwani hawana uhakika wa kurudi katika nafasi zao.
Wakati akizungumza na wazee wa jiji la Dar es Salaam wiki chache zilizopita, rais Magufuli alisema mojawapo ya sifa zitakazowarejesha viongozi katika nafasi za ukuu wa mikoa na wilaya, ni pamoja na ushiriki wao katika kumaliza au kushughulikia migogoro ya ardhi katika maeneo yao na kuondoa tatizo la madawati katika shule za msingi na sekondari za serikali.
Hadi mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na jumla ya wilaya 127 ambazo hata hivyo, zinaweza kuongezeka au kupungua kutokana na uamuzi binafsi wa rais kwani anayo mamlaka ya kikatiba ya kufanya hivyo pale anapoona inafaa.
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Greyson Msigwa hakuweza kuzungumzia suala la uteuzi huo akidai kuwepo katika kikao na badala yake akataka atumiwe ujumbe mfupi wa maneno, ambao hata hivyo baada ya kutumiwa hakuweza kuujibu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )