TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 23/06/2016
UTAFITI
MIEZI 8 TOKA MHE RAIS JOHN MAGUFULI AMECHAGULIWA KUWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu waandishi wa habari habari za leo na pole kwa majukumu mazito ya ujenzi wa Taifa. Taarifa yetu itajikita katika maeneo makuu mawili, Mkutano Mkuu wa CCM na UTAFITI wa Miezi 8 ya Mhe Rais John Magufuli.
Taasisi ya CZI ni taasisi huru isiyo ya kiserikali ambayo inajihusisha na ushauri wa mambo ya HABARI na kijamii, pamoja na tafiti mbalimbali. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, tulizunguka nchi nzima na kuuliza wananchi maswali ya papo kwa papo, ama kwa njia ya simu ama kwa kuhoji kimakundi kulingana na umri wa wahusika.
Tulihoji Watanzania 2,3oo wa kada mbalimbali katika maeneo kadha wa kadha tuliyotembelea kuanzia umri wa miaka 14 hadi 18 na kuanzia wenye umri wa miaka 18 hadi 30 na kuanzia miaka 30 hadi 60.
KUNDI LA 1 UMRI MIAKA 14-18
Kundi hili baada ya kuhojiwa wanaamini Rais John Magufuli ataleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, na atarejesha nidhamu ya masomo shuleni kuanzia shule za awali, msingi nasekondari kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 18.
Asilimia 78 ya vijana hao kwenye ngazi ya elimu ya msingi na sekondari wanaamini Mhe Rais Magufuli atasaidia kuleta mageuzi kwenye elimu ikiwa ni pamoja na kuondoa tatizo la madawati, mitaala na nidhamu ya walimu, huku asilimia 22 ya vijana hao wakisema Mhe Rais huenda asifanikiwe kwenye harakati zake za mageuzi kwenye sekta ya elimu. Pia kundi hili linaamini kuondolewa kwa michezo shuleni kutazidi kudidimiza maendeleo ya michezo nchini.
KUNDI LA II UMRI MIAKA 18-30.
Watanzania kuanzia miaka 18-30, asilimia 82 wanaamini serikali ya Rais Magufuli italeta mageuzi kwenye elimu hususan kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na kumaliza tatizo la mabweni ya kulala wanafunzi wa vyuo vikuu. Pia kada hiyo inaamini rais anaweza kupunguza tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na vijana nchini Tanzania. Sababu kuu ambayo inawafanya waseme hayo inatokana na kupambana na wafanyakazi hewa katika taasisi za serikali ambazo zimekuwa zikichangia kukosekana kwa ajira kwa vijana. Lakini sababu nyingine ya kuongezeka kwa ajira ni msimamo wa serikali wa kufufua na kuanzisha viwanda vipya, hasa vya mazao ya kilimo ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya kilimo.
Aidha asilimia 18 ya kada hii haiamini kama serikali ya awamu ya tano italeta mageuzi yoyote nchini na wanasema ni kawaida ya serikali kuwapa matumaini wananchi wake lakini mwishoni mambo hubaki vilevile kama awamu zilizopita.
KUNDI LA III UMRI MIAKA 30-60
Watanzania wenye umri wa miaka 30-60 waliohojiwa wanasema kuna uwezekano watumishi wa umma wakarejesha imani kwa serikali kutokana na juhudi za Mhe. Rais anavyopambana na ufisadi na rushwa kwa dhati.
Aidha kada hii asilimia 89.0 wanaamini Mhe Rais atamaliza matatizo ya wazee kwa kuanza kuwalipa posho kwa mwezi lakini pia wanaamini nidhamu ya watumishi itaongezeka miongoni mwa watumishi wa umma pamoja na binafsi kutokana na namna serikali inavyopambana na watumishi hewa na utumbuaji majipu unaoendelea kwenye serikali ya awamu ya tano.
Aidha kada hii inaamini umoja na mshikamano wa Watanzania utaendelea kuimarika na moyo wa kusaidiana kwa wananchi wa Tanzania utadumu na kuimarika pia.
Vile vile kada hii inasema Rais Magufuli anazidi kuwa maarufu huku wapinzani wakionekana kupoteza umaarufu kutokana na kushindwa kubuni mbinu mpya ya mapambano ya kisiasa.
Asilimia 11 ya kada hii inaamini serikali ya awamu ya tano haitaleta mageuzi yoyote kwa wazee na nidhamu kwa watumishi wa umma haitabadilika kutokana na aina ya viongozi wanaowasimamia watumishi hao ambao wengi wao siyo waadilifu na siyo watendaji na wafuatiliaji wa mambo kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa ujumla wake mhe rais anakubalika kwa asilimia 89% huku akiwa amewapiku Edward Lowasa na Mhe Jakaya KIkwete ambao wao wamegawana zilizobaki. Jakaya Kikwete akiwa na asilimia 7% huku Edward Lowasa akiwa na asilimia 4%.
Mikoa ambayo tulikwenda ni Dodoma, Mara, Geita, Ruvuma, Arusha, Manyara, Kusini Pemba, Wete Pemba, Kaskazini Unguja, Tabora, Kigoma, Pwani, Morogoro, Simiyu, na Tanga, na kuhoji wananchi takriban 2,300.
MAFANIKIO YA MIEZI NANE (8) YA UTAWALA WA RAIS DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI
Mara tu baada ya kutangazwa mshindi hata kabla ya kuapishwa Novemba 5, 2015 watu wengi walibeza kama angeweza kutekeleza yale aliyoyasema. Wapo waliosema kwamba asingeweza kupambana na rushwa na ufisadi kwa sababu mfumo huo umeanzia ndani ya CCM. Walizungumzia kuhusu suala la kufumua mfumo wa uendeshaji wa Serikali, kuijenga upya CCM, pamoja na namna ya kushirikiana na upinzani. Wengine wakahoji muundo wa baraza la mawaziri utakavyokuwa hasa kwa vile lililopita lilikuwa kubwa mno.
Hata hivyo, katika kipindi cha miezi nane tu, amefanya mambo makubwa mengi kana kwamba amekuwepo madarakani kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa hata ahadi zake nyingi amekwishazitekeleza na nyingine anaendelea kuzitekeleza. Tutajaribu kukumbusha machache kati ya mengi aliyoyafanya katika kipindi hicho.
Alielekeza Shs. 225 milioni zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya pongezi za Wabunge Dodoma kutumika kununua vitanda vya hospitali ya Muhimbili na Shs. 15 milioni tu ndio zitumike kwa ajili ya sherehe hiyo.
1. MPANGO MAHUSUSI WA KURUDISHA NIDHAMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA (UTUMBUAJI MAJIPU)
Kurudisha nidhamu kwa watumishi wa umma ilikuwa moja ya agenda zake na ahadi aliyoirudia Zaidi ya mara 100 wakati wa kampeni zake na hata sasa bado anaendelea kusema. Watanzania wamekuwa na kilio cha muda mrefu kwamba wamekuwa wakishindwa kupatiwa huduma muhimu na watendaji wa serikali, ambao wengi wao hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.
Itakumbukwa kwamba, hata kabla hajaunda Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli alifanya mambo makubwa kadhaa ambayo hayakutegemewa. Kwanza alifanya ziara mbili kubwa za kushtukiza ambapo Novemba 6, 2015 ikiwa ni siku moja tu baada ya kuapishwa alitembea kwa miguu kutoka Ikulu hadi Wizara ya Fedha ambako alipita katika ofisi moja baada ya nyingine na baadaye alifanya kikao na watendaji. Novemba 9 alifanya ziara nyingine ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alivunja Bodi ya Wakurugenzi, alimwondoa Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Hussein Kidanto na kuamuru mashine muhimu za vipimo za CT-Scan na MRI kutengenezwa haraka huku akitoa sehemu ya mshahara wake kumlipia mgonjwa mmoja aliyekuwa anahitaji kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.
Ni katika kipindi hicho ambapo Serikali, katika zile zile ziara za kushtukiza zilizofanywa na Rais mwenyewe na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Watanzania walishuhudia vigogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiswekwa ndani, kusimamishwa, kutenguliwa teuzi zao na wengine kufikishwa mahakamani kwa makossa mbalimbali, yakiwemo uzembe, rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Tumeona watendaji wa mamlaka nyingi za umma wakiendelea kusimamishwa/kufukuzwa kazi kama Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, UHAMIAJI na TRL. Hii imerudisha nidhamu kwa watumishi wa UMMA na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
2. MPANGO WA KUBANA MATUMIZI
Itakumbukwa kwamba, Rais Magufuli alipunguza kupunguza sherehe na dhifa za kitaifa na Jumatatu ya Novemba 23, 2015, alitangaza kufutwa kwa Sherehe za Uhuru Desemba 9 na kuagiza fedha za maandalizi ya sikukuu hiyo zitumike kutatua matatizo mengine, ikiwemo kufanya upanuzi wa Barabara ya Morocco-Mwenge huku akiagiza siku hiyo itumike kusafisha mazingira ili kupunguza matatizo ya kipindupindu nchini. Alifuta sherehe za Muungano na kuelekeza kwamba fedha hizo zitumike kupanua barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege jijini Mwanza hadi mjini. Aliagiza pia taasisi hizo zifanye vikao vyao katika kumbi maalum za idara zao badala ya kwenda mikoani ama kukodi kumbi za hoteli huku watu akijilipa posho nyingi wakati vikao hivyo ni vya kiutendaji tu.
Tumeshuhudia katika uteuzi wa viongozi wa serikali ya Awamu ya 5, Mh. Rais amezuia shamlashamla za kupongezana viongozi wa serikali wanapoteuliwa na kufanya uteuzi wa serikali ya awamu ya Tano kutumia bajeti ndogo katika siku hizo za uteuzi. Mfano, uteuzi wa Wakuu wa wilaya, Mawaziri na wakuu wa Mikoa hakukuwa na shamlashamla kama ilivyozoeleka katika awamu zilizopita.
Hili limesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zimekwenda kufanya shughuli za maendeleo ya wananchi. Wale waliodhani kwamba utendaji wa Dk. Magufuli ni mfumo wa kujilundikia majukumu bila utekelezaji (Slack Management Style) walikosea sana, kwa sababu tangu wakati ule tumeshuhudia watendaji wengi wazembe, wala rushwa na mafisadi wakiwajibishwa huku wengine wakifikishwa mahakamani.
3. WATUMISHI HEWA
Suala la kuwepo kwa watumishi hewa, ambalo lilikuwa linalalamikiwa kwa muda mrefu, safari hii Rais Magufuli alilitumbua ambapo tulishuhudia kwamba kumbe kulikuwa na watumishi hewa zaidi ya 12,000 waliokuwa wanalipwa mabilioni ya fedha ambazo ziliingia kwa maofisa wajanja. Kuonyesha kwamba hakuwa na mzaha hata kidogo, alimfuta kazi mara moja Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga baada ya kugundua kwamba alimdanganya kwamba mkoa wake haukuwa na mtumishi hewa hata mmoja wakati haikuwa hivyo. Mabilioni mengi ya fedha yameokolewa kutokana na zoezi hilo katika Serikali za Mitaa.
4. SAFARI ZA NJE KWA WATUMISHI WA UMMA NA VIONGOZI WA KISERIKALI
Rais Magufuli alianza mara moja kwa kutangaza kufuta safari zote za nje za mafunzo na ziara kwa maofisa na watendaji wa Serikali katika harakati za kubana matumizi huku akibainisha kwamba, safari hizo zililigharimu Taifa mabilioni ya fedha wakati nyingi hazikuwa na tija. Akasema yeyote ambaye alitaka kusafiri ilikuwa lazima apate kibali maalum kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au kwake yeye. Siyo siri kwamba hili limeondoa zile ‘safari za kufanya shopping’ ambazo maofisa wengi wa serikali walizitumia kutafuna fedha za umma na kuitia doa Serikali ya CCM.
Uamuzi wa Mh. Rais kurudisha utaratibu wa vibali vya kwenda nje, umeokoa pesa nyingi sana ambazo zilikuwa zinatumika na viongozi mbalimbali wa serikali kusafiri kwenda nchi za nje safari ambazo zilikuwa hazina tija kwa taifa. Kwa kulitekeleza hili hata yeye mwenyewe katika kipindi cha miezi 8 ya utawala amesafiri mara 2 tu, kwenda Rwanda na Uganda. Huu ni mfano ambao unatakiwa kuigwa na kuungwa mkono na watanzania wote walio na dhamana katika sekata ya umma.
5. ELIMU BURE (CHEKECHEA MPAKA KIDATO CHA NNE)
Katika kufuata Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, ameweza kupeleka TShs bilioni 18 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari. Hivi sasa tunashuhudia idadi kubwa ya udahili wa wanafunzi wa shule za msingi na kuongeza idadi kubwa ya uhitaji wa madawati hasa kwa shule za msingi. Wazazi wengi wameitikia na kuamua kupeleka watoto wao shuleni haya ni matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Elimu bure katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
6. PUNGUZO LA KODI KWA WAFANYAKAZI (PAYE) UKUSANYAJI WA MAPATO
Serikali makini hukusanya kodi! Rais Magufuli katika kipindi kifupi tu ameweza kusimamia vyema ukusanyaji wa kodi akianza kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wakwepaji sugu. Lakini pia Serikali imeweza kupunguza kiasi cha kodi ya PAYE kwa 2% katika mishahara ya wafanyakazi kila mwezi na kuondoa makali ya kodi kwa wafanyakazi wake.
7. VITA DHIDI YA MAFISADI
Mh. Rais pia ameweza kuanzisha mahakama ya mafisadi kwa lengo la kupambana na mafisadi ambao wamelifikisha taifa la Tanzania kwa wizi mkubwa wa mali za umma pamoja na matumizi mabaya ya fedha za serikali. Hili alilisema katika kampeni na amelitekeleza kwa asilimia 80 akionyesha dhamira yake ya kushughukia watu wa namna hiyo.
Katika sherehe za kuanza mwaka wa kimahakama Mh. Rais aliweza kuahidi na kutoa jumla ya Tshs Bilion 12 ili kuharakisha utendaji wa mahakama jambo ambalo halijawahi kufanyika na kila mwaka awamu zilizopita bajeti haitoshelezi kwa muhimili huu. Fedha hizo zilikabidhiwa kwa Idara hiyo mwezi Februari 2016.
Ajabu ni kwamba, kasi ya kuwawajibisha watumishi wa umma ikaanza kupingwa na baadhi ya wapinzani, hususan wale ambao walikuwa wanaahidi kwenye kamepni zao kwamba wangeweza kupambana na ufisadi! Siyo siri kwamba, tayari kasi yake hiyo ilikuwa imewapoteza wapinzani hata kabla hajaunda baraza la mawaziri – wakati huo akiwa na wasaidizi watatu tu – Katibu Mkuu Kiongozi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu!
8. UJENZI WA MABWENI KWA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Mh. Rais amehaidi kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam jambo ambalo lilipigiwa kelele sana na wanafunzi katika awamu zilizopita lakini leo litafanyika kupitia Mh. Rais wa awamu ya Tano kama alivyo ahidi.
Yako mengi sana aliyoyatekeleza ambayo hayawezi kutosha hapa, lakini Rais Magufuli, ambaye kimsingi ameisongesha mbele Tanzania katika kipindi kifupi, anaweza kufanya mambo makubwa zaidi hasa atakapokabidhiwa uenyekiti wa taifa wa CCM, chama tawala na kikongwe kabisa barani Afrika, kwa sababu huko nako ataondoa mfumo mbovu wa uongozi unaokifanya chama hicho kilalamikiwe na kiwe agenda kuu ya wapinzani kila mara.
Wale wanaobeza utendaji wake wanapaswa kukaa kimya, kwani Wananchi waliomweka madarakani ndio watakaompima na kumhukumu, kwa sababu hakuna aliyetegemea kama serikali hii ingeweza kuondoa Service Charge kwenye umeme wa majumbani ambapo wananchi walikuwa wanaumizwa sana na hili jambo.
Mwenye nia njema na maendeleo ya taifa hili, anapaswa kuiunga mkono kwa dhati kabisa serikali ya Dk. Magufuli kwa utendaji huu na siyo kumhujumu, kumbeza ama kutoka visingizio vyovyote vile.
KUELEKEA MKUTANO MKUU WA CCM TAIFA JULAI 23 MWAKA HUU.
Ndugu zangu Watanzania, wakati wanachama wa CCM wakijiandaa na Mkutano Mkuu wa chama hicho kikiwa na ajenda moja tu kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa CCM, wanachama wa chama hicho wanapaswa kutambua mambo kadhaa ambayo yanampa umuhimu wa kipekee Rais Magufuli kupewa nafasi hiyo na wajumbe wa mkutano mkuu, pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Chama cha Mapinduzi kina rasilimali nyingi:
1. Rasilimali watu
2. Rasilimali Ardhi, Majengo na Viwanja
3. Wananzuoni wa kila taaluma
4. Wafanyabiashara ndogondogo (machinga)
5. Wafanyabiashara wa kati na wakubwa
6. Wanachama wake wanaozidi milioni 9
7. Mashabiki wake wanaozidi milioni 28.9
8. Wakulima
9. Wavuvi
10. Wafugaji nk.
Lakini pamoja na utajiri huo, bado chama hicho hakiwezi kujiendesha na wanategemea Ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, pamoja na wafadhili ambao wengine siyo wasafi kwenye rekodi za kodi.
Ndugu waandishi wa habari, baada ya kutafakari kwa kina tumegundua kwamba, Mhe Rais Magufuli anazo agenda nzuri za kukiendeleza chama hicho kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo pindi atakapopewa chama hicho.
Agenda hizo ni:
Mosi: Kuhakikisha chama kinajitegemea kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo itakifanya kijiendeshe chenyewe bila kutegemea wafadhili.
Pili: Miradi ambayo ipo tayari ijulikane na iwekwe wazi na iwanufaishe wanachama na wananchi kwa ujumla.
Tatu: Kuongeza wanachama zaidi wa chama hicho.
Nne: Kuwa na wanachama wanaokipenda chama hicho na wenye uzalendo na chama hicho na nchi yao.
Ndugu waandishi wa habari, kwa mtazamo huo tunawaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu waone umuhimu wa kumpa Mhe Rais Magufuli kura za kutosha ili awe mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Aidha, kuna taarifa za baadhi wa wanaCCM wachache ambao wamekuwa wanazunguka mikoani na wilayani wakieneza taarifa za uongo kwamba Rais Magufuli mwenyewe ndiye hataki kuwa mwenyekiti wa chama.
Ndugu wananchi na waandishi wa habari, tunawaonya hao wanaoeneza uongo huo waache mara moja kwa kuwa uongo na uzushi huo haulengi kukijenga chama na watu hao huenda wakajikuta kwenye wakati mgumu kama wataendelea kuzusha na kueneza uongo huo.
Tunawaomba Watanzania wazidi kumuombea rais wetu kwa kuwa anaonyesha nia ya dhati kuhakikisha nchi inapata maendeleo, kwani hata wakati aliposhiriki jubilee ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania alisikika akiwataka benki kuu kuhakikisha wanalinda thamani ya shilingi pamoja na kushusha mfumko wa bei.
Kama mnavyojua, moja ya matatizo makubwa kwa watanzania hasa wa kipato cha chini ni mfumko wa bei ambao umekuwa unawatesa kila mwaka bila serikali kutafuta njia mbadala za kupunguza mfumko huo, lakini rais wa awamu ya tano Mhe Magufuli na serikali yake wanapambana kuondoa kero hiyo kubwa kwa Watanzania.
Tudumishe umoja, mshikamano na Amani. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeandaliwa na:
David Saire Manoti-Mwanasiasa Kijana
Raphael Nyang’i Awino- Mwanasiasa kijana
Cyprian Musiba Nyamagambile- Mwandishi/Mtafiti
Dotto omary Nyirenda - Mwanadiplomasia kijana
Daniel Mahelela - Mtafiti
Juma George Chikawe-Mwanasheria
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )