Kwa muda mrefu nimekuwa nikitoa hamasa kwa vijana wenzangu wa kike na kiume na watu wa kada mbalimbali, wito wangu umekuwa nikuwataka vijana wenzangu kauanza utamaduni wa kuwekeza kwa muda mrefu na kujifunza ujasiriamali. Ninaandika makala hii kutoa ushuhuda wa niliyoyafanya kwa muda wa zaidi ya miaka miwili iliyopita na kuniletea mafanikio makubwa.
Nilianza kujishighulisha na ujasiriamali nilipokuwa chuo kikuu mwaka wa pili, kwa kuuza vocha na kazi ya ‘steshenari’ na uuzaji wa laptop, sikuendelea nazo sana kwa sababu ya kubanwa na masomo yachuo. Nilipomaliza chuo 2010, nilianza kilimo cha mboga na kufuga kuku hapa Iringa mjini, baada ya hapo kaka yangu alianza kunihimiza kuhusu kilimo cha miti ambacho yeye mwenyewe anafanya.
Na baadaye nikakutana na rafiki yangu Albert Sanga ambaye pia anajishughulisha sana na kilimo cha miti. Tangu 2011 nilinunua shamba la ekari 10 na kuzipanda miti hela ambayo niliipata baada ya kuuza matango niliyolima kijijini Kalenga, nikaongeza bidii zaidi ya kulima matango na kununua mashamba, leo nina ekari nyingi.
Albert sanga, mjasirimali na mwekezaji alipata kuandika haya kuhusu mimi:- “UNASUBIRI UPATE MTAJI? OPSss! UNAWEZA KUFA MASIKINI! Nina rafiki yangu mpambanaji kweli kweli na msomi wa chuo kikuu wa mambo ya maendeleo na elimu; na mtaalamu wa IT, anaitwa Meshack Maganga. Wakati fulani huko nyuma alinifuata na kuniambia, "Sanga nimeamua kuanza kui-invest katika mashamba ya miti; mtaji wa kuanzia nina tsh elfu ishirini na tano, (25,000?/=).
Nikamwambia "Kupata ekari moja si chini ya laki sita na wewe una tsh 25,000/= utawezaje?" Akanijibu "Nitaweza!", Sikumwelewa! Kumbe alikuwa anaona mbali! Alichofanya alichukua hiyo 25,000/= akaenda nayo eneo moja linaitwa Kalenga (km 20 kutoka Iringa mjini) huko akalima matango. Angalia mchanganuo: Shamba nusu eka akakodi kwa tsh 10,000/=, mbegu za matango akanunua Tsh. 7,000/=.
Kwenye kulima akalima kwa mikono yake akisaidiana na kibarua mmoja. Fedha iliyobaki 8,000/= akalipa kibarua na kununulia dawa ya kuua wadudu. Alipokuja kuvuna akapata tsh 800,000/= (laki nane). Alipokuja na fedha hii tukaenda kutafuta shamba la miti akaanza na ekari moja huku pesa nyingine akairudisha shambani.
Hivi leo Bw. Maganga ana ekari zisizopungua hamsini za mashamba ya miti na anaendelea na kilimo cha umwagiliaji. Lakini HAPO amefika kwa kutumia tsh 25,000/= tu. Tunaposema hauhitaji mamilioni kujiajiri tunatamani ujifunze kutoka kwa waliofanikiwa kama Bw. Maganga. Unaweza kumwandikia” Akaendelea kwa kusema:-
Kuhusu kilimo cha miti ninacho kifanya mimi na nimepania kwelikweli ndani ya nchi yangu niipendayo Tanzania ni kwamba, kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira. Katika Tanzania mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu inayoongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa.
Miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea pamoja na utengenezeaji wa karatasi. Ukiacha mahitaji haya tuliyoyazoea; hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya ambapo mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ukaa. Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae uvune mbao, nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi.
Hii ni sawa na kutegeneza hela ukiwa umelala. Mbali na kuuza hewa ukaa, vile vile unaweza kufuga nyuki na kuendelea kuvuna asali wakati unasubiri kukusanya mamilioni kwa kuuza miti ya nguzo, karatasi ama mbao.Kilimo hiki cha miti ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (middle& long term investments). Kiutamaduni watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji wa muda mrefu.
Hata hivyo kama una mpango wa kuwa na “financial freedom” usikwepe kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema “Information is power”. Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa taarifa tu. Kazi yangu leo ni kukupa taarifa hizi za utajirisho. Miti ya mbao inatumia wastani wa miaka sita hadi 8 au saba, tangu kupandwa hadi kuvunwa kwake.
Hii ina maana inapofikisha umri wa miaka sita huwa tayari kwa kuanza kuvunwa kwa mbao ndogo. Ekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti mia sita (600). Wastani wa chini wa mti mmoja kwa sasa uliokomaa ni shilingi elfu ishirini (30,000 hadi 60,000,inategemea na ukubwa wa mti). Ina maana katika ekari moja ukiwa na miti iliyokomaa unakusanya jumla ya shilingi milioni kumi na nane (18,000,000).
Fedha hiyo (kadirio la chini kabisa) utaipata ikiwa unaamua kuuza kwa bei ya jumla miti ikiwa shambani. Lakini kama ukiamua kupasua mbao wewe mwenyewe unaweza kuvuna mbao hadi za milioni thelathini na mbili (32,000,000) kwa ekari moja. Hadi sasa uhitaji (demand) wa mbao katika soko ni mkubwa kuliko ugavi (supply) hivyo kwa miaka 10 ijayo hatutarajii kushuka kwa soko la mbao, nguzo ama malighafi za karatasi.
Gharama ya kununua shamba tupu ni kati ya shilingi laki moja na 20 elfu (120,000) na laki moja, kutegemea na maeneo husika unayotaka ama kupata. Gharama za kuandaa shamba, kununua miche na kupanda ni kati ya shilingi laki moja na nusu,na laki moja. Hii ina maana unaweza kumiliki ekari moja ya msitu wa miti kwa hadi shilingi laki sita tu! Kutegemea na umri wa miti unayotaka.
Mtu unaweza kuona kuwa pengine kununua shamba tupu na kuanza kuhangaika na upandaji miti itakuwa ni mlolongo mkubwa; kukusaidia katika hilo nimekuwa na utaratibu wa kumilikisha mashamba yenye miti (kuuza) kwa bei nafuu sana. Yapo mashamba yenye miti ya kuanzia mwaka mmoja, miaka miwili, miaka mitatu na miaka minne.
Uponunua mashamba haya kutoka kwangu, mimi naendelea na upandaji wa mashamba mapya kupitia fedha hizo. Kilimo cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi mkubwa sana na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba/mradi muda wote. Kuna kazi chache ambazo zinahitajika ukishapanda shamba lako.
Mvua inyeshe ama isinyeshe mti wa mbao, nguzo ama karatasi ukishachipua huwa haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini. Kazi namba moja unapokuwa umeshakamilisha upandaji wa miti kwenye shamba; ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka, kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja (prooning).
Gharama zote hizo yaani kutengeneza njia za moto, kufyekea na kulinda moto haizidi laki mbili kwa mwaka mzima. Kwa maana hii gharama za kuhudumia shamba la miti ekari moja kutoka kupandwa hadi kuvunwa ni wastani wa shilingi milioni moja tu. Gharama hizi ninazopiga ni ikiwa utaamua kununua shamba leo na kama ungekuwa tayari una shamba ambalo unalihudumia leo.
Hata hivyo nadhani wote tunafahamu kuwa ardhi ni rasilimali inayopanda thamani kila siku. Vile vile tunatambua kuwa suala la mazingira ni tete kwa sasa na katika karne zijazo kama wataalamu wanavyotuthibitishia. Hii ina maana kuwa ukiwa na shamba la miti leo; thamani ya ardhi hiyo inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda inazidi kupanda thamani kila kukicha.
Jambo la uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti, mbao, nguzo itayumba hutaweza kupoteza mtaji uliotumia na wala hutakosa kuzalisha faida kwa shamba utakalokuwa umemiliki, iwe ni eka moja, kumi, mia ama elfu moja. Mbali na hivyo unaweza ukaona, ahaa, miaka sita hadi kumi ni mingi mno; bado una nafasi ya kupata faida hata ndani ya mwaka mmoja, miwili au mitatu.
Ukishapanda shamba la miti ekari moja kisha baada ya mwaka mmoja ukaamua uuze utauza si chini ya milioni mbili hadi nne. Kukusanya milioni nne kwa mtaji wa laki sita, pasipo kutumia muda mwingi ama usumbufu wa kusimamia; hakika ni faida nono.
Huenda hadi kufika hapa unaweza ukawa umeshavutiwa na biashara hii. Wengi wenu mnaweza kujiuliza maswali mkubwa mawili; “Ninatamani nifanye mradi huu lakini Iringa sikufahamu na hata kama nakufahamu nitaanzia wapi kupata hayo maeneo?” Pili: Niko mbali na sina muda wa kushinda Iringa, Je, ni nani atanisaidia kupanda, kusimamia na kuendesha hayo mashamba?
Ili kutimiza ndoto yangu hiyo nimeweka utaratibu ufuatao utakaohakikisha kila mwenye ndoto, kiu na hamasiko la kuwekeza kwenye kilimo cha miti anafanikiwa. Jisikie huru wakati wowote kuwasiliana nami kwa ufafanuzi na msaada wa fursa hii. Natamani watanzania tuache kulalamika kuhusu wageni kuvamia ardhi yetu, badala yake tuchangamke kumiliki na kufanya uzalishaji katika ardhi yetu.
Inawezekana! Kwa kutumia sheria ya ardhi ya mwaka 1999 sheria namba 5 utapata documents za umiliki; kwa kuzingatia taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana na umilikaji ardhi nitahakikisha nakusaidia ili ndoto yako itimie.
Yupo Baba yangu anaishi Mafinga ambae siku za karibuni amepewa Tuzo ya Rais kwa kuwa mpandaji namba moja wa miti na utunzaji wa mazingira, ameahidi kutoa msaada kwa Mtanzania wa ndani na nje ya Tanzania kumsadia kupata eneo la kupanda miti na kauli ya siku zote ni “USIKUBALI KUWA MNYONGE WA KIUCHUMI NDANI YA TANZANIA.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )