Nape ameeleza kuwa uamuzi huo uliwasaidia kwa kiasi kikubwa kwani mwanasiasa huyo aliyekuwa na nguvu kubwa ndani ya chama hicho alikuwa alama ya ufisadi kutokana na kukabiliwa na tuhuma nyingi za ufisadi.
“Lowassa alikuwa alama ya ufisadi, alipoondoka aliturahisishia kazi. Watu walikuwa wanahusisha ufisadi na umasikini, walichoka na walikuwa radhi kuchagua hata jiwe lakini sio CCM,” alisema Nape.
Alisema kuwa angepata nafasi ya kumshauri Lowassa katika siasa, angemshauri ajiuzulu siasa kabla hajaondolewa kwa aibu katika medani za siasa.
Kadhalika, Nape alisema kuwa kosa kubwa ambalo lilifanywa na vyama vya upinzani ni kumpokea Lowassa ambaye amedai alikuwa amesababisha CCM kupakwa matope ya uchafu kutokana na kuwa na tuhuma nyingi.
Hata hivyo, Nape alimpongeza Lowassa kwa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu kwa kuwa uamuzi huo ulisaidia kuliweka Taifa katika hali ya amani baada ya uchaguzi.
Lowassa amekuwa akikanusha tuhuma zote zilizokuwa zikielekezwa kwake hususan tuhuma za kuhusika na sakata la Richmond lililosababisha ajiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Alijiunga na Chadema na kugombea nafasi ya urais akiungwa mkono na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa.
Alipata kura takribani milioni 6 na kusaidia kupata wabunge wengi zaidi wa upinzani akiweka historia ya ushindani mkubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye uchaguzi mkuu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )