Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya,Roshanara mwenye umri wa miaka 23, alishinda taji la mwaka uliopita na alikuwa anatarajiwa kuiwakilisha Kenya kwenye mashindano ya Miss World, mwishoni mwa mwaka huu.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, wasimamizi wa Miss World Kenya, kampuni ya bidhaa za urembo, Ashleys imeandika,
'Kuanzia sasa, Roshanara hatoiwakilisha Kenya nchini na hata kimataifa kama Miss World. Tumefahamishwa kuhusu sakata kubwa inayomkumba Roshanara Ebrahim, ambayo inakiuka sheria na masharti ya Miss World Kenya. Tunatekeleza sheria zetu na tunatarajia wanamitindo wetu kusimamia maisha yao ya kibinafsi.
Kulingana na gazeti hilo , Roshanara ameandika kukubaliana na uamuzi huo na kuwasihi warembo wenye umri mdogo kuhakikisha maisha yao ya kibinafsi, hayaathiri jukumu lao la Miss World.
''Nakaribisha uamuzi wa ofisi ya Miss World Kenya kunipokonya taji la Miss World Kenya kwa masikitiko makubwa, namtakia atakayechukua nafasi yangu kila la heri.
Kabla ya uamuzi wa ofisi ya Miss World Kenya, Roshanara alilazimika kujitetea dhidi ya madai yaliomhusisha kuwa na uhusiano na mwanasiasa mashuhuri.
Tayari ofisi ya Miss World Kenya, imeahidi kumtangaza mwanamitindo atakayejaza pengo lililoachwa na Roshanara Ebrahim siku chache zijaazo.
Roshanara anayesomea uwakili, anatarajiwa kuendelea na shughuli zake za kuwasaidia watoto walio na mpasuko wa mdomo, yaani 'cleft.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )