WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Jiji
la Mbeya baada ya kuwepo kwa ubadhilifu katika ujenzi wa soko la
Mwanjelwa.
“Inasikitisha
ujenzi wa soko hili kuingia ubabaishaji. Ujenzi wa soko ungegharimu sh
bilioni 16 ila sasa watendaji wamefanya mambo ya hovyo na kufikia sh
bilioni 26 hatuwezi kuwavumilia lazima hatua zichukuliwe kwa wote
watakaobainika katika ubadhilifu huu,” alisema.
Pia
amempa siku tatu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla kufanya uchunguzi
na kubaini nani aliyetafuna sh milioni 489 zilizotolewa na Benki ya CRDB
kwa ajili ya uendelezaji wa soko hilo ambazo hazijulikani zilipo.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 09, 2016) wakati alipofanya
ziara ya kushitukiza katika soko la Mwanjelwa na kubaini ubadhilifu wa
fedha katika ujenzi wa soko hilo.
Waziri
Mkuu amesema mara baada ya CAG kumaliza kufanya ukaguzi atatoa taarifa
na mtu yeyote atakayetajwa katika ripoti hiyo kuwa amehusika na
ubadhilifu huo atawajibika hata kama yuko nje ya Jiji la Mbeya.
Alisema
kitendo cha kuongeza gharama za ujenzi wa soko hilo kutokana na
kuchelewa kwa ujenzi wake kinaisababishia Halmashauri yaJiji kulipa sh
milioni 200 kila mwezi kwa ajili ya marejesho, hivyo aliagiza
aliyesababisha gharama hizo asakwe na achukuliwe hatua kali ili iwe
fundisho kwa wengine.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa Mbeya, Amos Makalla
kuhakikisha mtu aliyepangishwa katika kibanda cha kukusanyia uchafu
sokoni hapo anaondolewa haraka na kurudishiwa fedha zake ili kibanda
hicho kitumike kama ilivyokusudiwa.
Pia
alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kufanya ukaguzi katika vyumba vya maduka
sokoni hapo na ifikapo Jumatatu mtu hajaweka mali anyang’anywe na
kupangishwa kwa mtu mwingine mwenye kuhitaji.
Alisema
hayo baada ya baadhi ya wafanyabiashara kulalamika kuwa kuna watu
wamechukua vyumba vingi vya maduka kwa ajili ya kuvipangisha kwa
wafanyabiashara kwa gharama kubwa tofauti na inayotozwa na Halmashauri,
hivyo kunyima nafasi kwa walengwa kunufaika na soko hilo.
Mmoja
wa wajasiriliamali sokoni hapo Mohammed Said alisema watu wameshika
vyumba na kuviuza kwa sh milioni 20 hadi 40 kulingana na eneo kilipo
chumba jambo linalosababisha baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kupata
nafasi katika soko hilo.
Awali
Mkuu wa Mkoa alisema soko hilo linakabiliwa na matatizo mbalimbali
kwani hata wahanga waliokuwa wanafanya biashara kabla ya soko kuungua
moto hawakupewa kipaumbele wakati wa upangishaji wa vyumba vya maduka.
Kuhusu
suala la kukosekana kwa wateja sokoni hapo Makalla amewataka
wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyokuwa
rasmi kuhamia sokoni hapo mara moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 08, 2016.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )