Wabunge wote wa Chama
cha Wananchi (CUF) wametangaza rasmi kutomtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa
chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wamemtaka Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutomkumbatia mwanasiasa
huyo aliyebobea katika uchumi, ikielezwa kwa sasa hana sifa za kuwa
mwenyekiti wa chama hicho, labda aanze upya mchakato.
Wameeleza msimamo huo
jana mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali ambaye pia
ni Kiongozi wa Wabunge wa CUF katika mkutano baina ya waandishi wa
habari za Bunge na wabunge wa CUF isipokuwa Mbunge wa Jimbo la Kaliua,
Magdalena Sakaya aliyesimamishwa uanachama, ingawa anaendelea kutimiza
majukumu yake bungeni.
Mngwali alisema Profesa
Lipumba amekuwa akijaribu kukiyumbisha chama na hivi karibuni kudai
amekaririwa akisema anasubiri barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya
kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.
“Wakati anajiuzulu
uenyekiti Agosti 5, mwaka jana aliutangazia umma na kudai anakwenda
Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili aje kuisaidia serikali, lakini
inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti. Hilo hatukubali kwa
kuwa chama kina taratibu zake,” alisema.
Aliongeza kuwa,
alikiacha chama katika wakati mgumu kuelekea Uchaguzi Mkuu, lakini
kikaimarika zaidi kwa kupata wabunge 43, madiwani 287, kuongoza manispaa
mbili na halmashauri za wilaya tatu, hivyo wanashangazwa kuona akitaka
kurejea, tena kwa kutumia nguvu.
“Tunataka ifahamike kwa
dhati kuwa, sisi wabunge, hatumtambui tena Profesa Lipumba kama
Mwenyekiti wa CUF,” alisema Mngwali na kumtaka Msajili kutomuidhinisha
Lipumba, kitendo alichodai kitachochea mgogoro ndani ya chama.
Aliongeza kuwa badala ya
kutumia mabavu kutaka kurejea madarakani, ni vyema akabaki na heshima
yake, kwani amekitendea mambo mengi chama hicho na kwamba wanamheshimu,
hivyo afuate taratibu za kichama kutaka kuwania tena uenyekiti.
Mngwali alisema
wamekubaliana na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF wa kuwasimamisha
uanachama Lipumba na wenzake tangu Agosti 28, 2016 kutokana na kile
kinachodaiwa kukiuka Katiba ya chama hicho.
Miongoni mwa tuhuma zao
ni kusababisha vurugu wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Uchaguzi Agosti
21, mwaka huu jijini Dar es Salaam uliokuwa unalenga kumthibitisha Juma
Duni Haji kuwa Mwenyekiti mpya.
Hata hivyo, kutokana na
vurugu zilizoibuka, mkutano huo ulivunjika. Mbali ya Lipumba na Sakaya,
wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya ambaye alikuwa
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura Mustapha, Omar
Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub
Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura ni mjumbe wa
Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya
Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi cha 2010/2015,
Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake,
kisiwani Pemba.
Kutokana na kusimamishwa
kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui
alimtangaza Julius Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa
kiongozi wa Kamati ya Uongozi wa muda inayowajumuisha pia wabunge Katani
Ahmed Katani na Savelina Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )