Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametoa onyo kwa
viongozi wa Serikali na hasa anaowateua kuwaheshimu na kuzingatia
maagizo yanayotolewa na viongozi wa chama hicho, vinginevyo
atawachukulia hatua.
Dk
Magufuli aliitoa kauli hiyo jana mara mbili alipokuwa anafungua mkutano
mkuu wa chama hicho asubuhi na akairudia tena alipokuwa anaufunga
usiku.
Katika
mkutano huo uliofanyika siku nzima na kuonyeshwa muda wote moja kwa
moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Magufuli alichaguliwa na
wajumbe wa mkutano huo kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka
mitano baada ya kupigiwa kura zote 1,828 katika ukumbi wa Jakaya
Kikwete.
“Viongozi
wa Serikali wanapaswa kutambua kwamba viongozi wa CCM ndio hasa
wanaostahili. Kiongozi wa Serikali wa cheo chochote anawajibika kwa
viongozi wa CCM,” alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa
wajumbe wa mkutano huo.
“Viongozi
wa Serikali katika ngazi yoyote watambue kuwa waajiri wetu wakuu ni
CCM, mimi bila CCM nisingekuwa Rais, CCM ndiyo kimejadili jina langu.
Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM na wenye ilani hiyo ni
hawa hapa (wajumbe) nendeni mkawasikilize,” alisema.
Dk Magufuli alionya asijitokeze kiongozi yeyote wa Serikali wa kusema hayajui (mambo) ya CCM.
“Kama mimi Rais niliyewateua ninayajua ya CCM asitokee mtu yoyote akasema hayajui mambo ya chama changu,” alisema.
Hata
hivyo, alisema kauli hiyo isiwavimbishe kichwa viongozi wa CCM na
kufanya mambo kinyume wakitegemea uongozi wao ndani ya chama hicho
tawala.
“Nataka
viongozi wa CCM kuheshimu viongozi wa Serikali na viongozi wa Serikali
kuheshimu sana sana sana viongozi wa chama,” alisisitiza.
Katika
mkutano huo, Magufuli alichaguliwa kwa kupata kura zote 1,828, huku
makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula akichaguliwa kwa kura
1,827. Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
akichaguliwa kwa kura 1,819.
Viongozi hao watatu walichaguliwa kwa kupata asilimia 100 ya kura zilizopigwa.
Mkutano huo pia uliwachagua wajumbe 30 wa Halmashauri Kuu (NEC) kati yao 15 kutoka Tanzania Bara na 15 wa Zanzibar.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )