BALOZI
wa China hapa nchini, Wang Ke amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko
tayari kushawishi taasisi za fedha ikiwemo Benki ya EXIM ya nchini humo
kushiriki ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya
kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa mradi huo.
Alisema
kuwa kutokana na ukubwa wa mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za
Marekani bilioni 7.6 hadi kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi
yakinifu ili kukidhi masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na
taasisi nyingine zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu.
“Mradi
huu ni muhimu na wa kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa
kuona mradi huo unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo
na abiria na kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara
kwa kuwa shehena kubwa ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo.
Aidha,
Balozi Ke alisema kuwa nchi yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu
za ndani kati yake na Tanzania ili mradi wa reli ya TAZARA uanze ili
kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania
na Zambia pamoja na nchi za maziwa makuu.
Balozi
Ke alitumia fursa hiyo kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano kwa kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za
umma, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.
Akizungumza
mara baada ya mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa
kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
Kimataifa (SGR) ili China kupitia taasisi zake iweze kujenga sehemu ya
mradi huo.
“Tayari
mradi umeanza kujengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwahiyo
kujitokeza kwa China kutaka kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia
kukamilisha mradi huo muhimu kwa haraka na kwa wakati” Alisema Dkt.
Mpango.
Alisema
pia kuwa China imeonesha nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa
Dodoma kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa kupanga miji ambapo nchi
hiyo imeonesha nia ya kujenga miundombinu ya elimu, barabara, uwanja wa
ndege wa kimataifa-Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka
pamoja na majengo ya kisasa.
Kuhusu
biashara, Dkt. Mpango alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia
Tanzania kukuza kiwango cha biashara ambapo takwimu zilizoko zinaonesha
kuwa urari wa biashara kati ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa
ikinunua bidhaa nyingi kutoka nchini humo kuliko inavyo uza bidhaa na
huduma zake.
“Mwaka
2016 Tanzania iliuza China bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za
marekani milioni 460 wakati China iliuza hapa nchini bidhaa zenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa
karibu mara 5 ya kile tulichowauzia” Alisema Dkt. Mpango.
Ili
kuvutia Sekta ya utalii, Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya
ndege wa moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii
wengi kutoka nchini humo na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya
usafiri wa anga iweze iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na
hivyo kufanikisha jambo hilo.
“China
imeandaa maonesho makubwa ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma
mbalimbali mwezi Novemba, 2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja
na Bodi ya Utalii nchini wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye
maonesho hayo ili kutumia nafasi hiyo kujitangaza” Alisistiza Dkt.
Mpango.
Aidha,
Dkt. Mpango alieleza kuwa Balozi Wang Ke, amesema kuwa Nchi yake
itashiriki katika ujenzi wa miradi ya bandari ili kukuza masuala ya
usafiri kwa kuboresha bandari za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar
es Salaam, Mtwara na katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Waziri
huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alitoa wito kwa wawekezaji
kutoka China na nchi nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki
ambacho Tanzania inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Miradi
mikubwa ambayo China imewekeza na kufadhili hadi sasa hapa nchini ni
Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Urafiki, ujenzi wa barabara, majengo, ujenzi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi dar es Salaam, Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dare Salaam, Ujenzi wa Mabweni ya
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miradi mingine kadha wa
kadha.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )