Watu
sita wanashikiliwa na polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za kukutwa na
vipande vitatu vya mifupa ya mtu wanayedai kuwa ni albino, pamoja na
mafuta na ulimi unaodhaniwa kuwa wa simba.
Kamanda
wa polisi mkoani hapa, Mathias Nyange alisema jana kuwa watu hao
walikamatwa juzi saa 7:00 mchana katika mji wa Tunduma wilayani Momba na
askari waliokuwa doria.
Alisema
watuhumiwa hao walikutwa na mafuta ya simba, mifupa mitatu ya albino,
mfupa mmoja wa mnyama ambaye hajajulikana, na vipande viwili vya ulimi,
vitu vinavyosadikiwa kuwa ni vifaa vya tiba asili.
Kamanda
Nyange alidai kuwa baada ya kuhojiwa, watuhumiwa walikiri kuwa mifupa
waliyokutwa nayo ni ya albino waliyemkata mkono mkoani Morogoro.
Alisema
kati ya watuhumiwa hao wawili ni wakazi wa Morogoro, wawili wakazi wa
Mbozi, mmoja ni mkazi wa Wilaya ya Momba na mwingine ni kutoka Nakonde
nchini Zambia.
Nyange alisema watuhumiwa hao wanatarajia kupelekwa mkoani Morogoro ambako ndiko wanakotuhumiwa kutenda kosa.
Wakati
huohuo, Nyange amesema watu watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati
ya miaka 25 na 30 wamefariki dunia baada ya kupigwa risasi na askari
waliokuwa doria saa 4:00 usiku wa Novemba 30 baada ya kukaidi amri ya
kusimama ya polisi ambao waliwatilia shaka.
Baada
ya kukataa kutii amri ya kusimama, polisi waliwafuatilia na baadaye
watu hao walianza kuwafyatulia risasi, jambo ambalo kamanda huyo alisema
liliwalazimisha askari kuanza kujibizana nao.
Alisema
baada ya kuwapekua walikutwa na silaha moja aina ya bastola
iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za short gun ikiwa na risasi
moja na pia walikutwa na mapanga mawili pamoja na kipande kimoja cha
nondo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )