SERIKALI
haijatoa ruhusa kwa Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya
‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Baadhi ya mitandao ilitoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: “Waziri Mkuu aruhusu kozi za ‘Foundation’ Chuo Kikuu Huria”
kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017)
wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali
ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.
Akizungumza
na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa
Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanyia
maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.
“Kwa
sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera
tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu
wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” alisema.
“Programu
kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia
kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu
wanaendelea kuiboresha. Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa
Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote ili
kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” alisema.
Mapema,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda
alisema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi
za Foundation katika chuo hicho.
“Tayari
tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi
matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri mrejesho
kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” alisema Prof.
Bisanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )