Askari wa Tanzania aliyejeruhiwa katika shambulizi lililoua wengine 14 walio katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ameripotiwa kufariki dunia.
Kifo hicho kinaongeza idadi na kufikia waliouawa katika shambulizi hilo kufikia 15. Askari 44 walijeruhiwa.
Umoja wa Mataifa (UN) umeelezea shambulizi hilo ni tukio baya zaidi lililovikumba vikosi vyake katika kipindi cha miaka 25.
Pia, UN imetuma rambirambi kwa Serikali ya Tanzania na ndugu waliopoteza wapendwa wao.
Katika
ujumbe wa Twitter, ujumbe maalumu wa UN ulio DRC (Munusco) umesema
askari huyo ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulizi la Desemba
7,2017.
Hakuna
taarifa zaidi zilizotolewa mbali ya kueleza kuwa, “Umoja wa Mataifa
umehuzunishwa na kusikitishwa kutokana na mauaji hayo.”
Mashambulizi hayo yanadaiwa kufanywa na wapiganaji wa kundi la ADF waliojichimbia katika misitu ya Congo.
Umoja wa Mataifa umeanza uchunguzi kwa kina kuhusu shambulizi hilo na umeahidi kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.
Mkuu
wa operesheni za ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre
Lacroix amesema uchunguzi unafanywa kwa kuzingatia vigezo vyote vya
kimataifa.
Amesema baada ya kukamilika wataalamu watafanya uchambuzi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuzuia mauaji kama hayo kujirudia.
“Uchunguzi
utafanyika kwa mbinu ambazo zinatakiwa. Hitimisho na mapendekezo
yatachambuliwa kwa kina na kuzingatiwa kwa hali ya juu na kwa haraka
iwezekanavyo,” amesema baada ya kutembelea kambi ya Semuliki iliyoko
Kivu Kaskazini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )