Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa atasimamia kwa nguvu zote
masuala yote yanayohusu maendeleo, kudumisha Muungano wa Tanzania Bara
na Tanzania Zanzibar na kudumisha amani kwa faida ya wananchi.
Rais
Magufuli amesema hayo jana tarehe 03 Septemba, 2016 alipokuwa
akizungumza na wananchi wa Zanzibar katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika uwanja wa Kibandamaiti Mjini Unguja.
Dkt.
Magufuli ambaye aliongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alisema ili
mambo hayo yafanikiwe Wananchi wa Zanzibar hawana budi kukataa
kujihusisha na vitendo vya vurugu na kuvunja amani na amewaonya watu
wanaochochea vitendo hivyo kuacha mara moja.
Aliwataka
wananchi wa Zanzibar kujihadhari dhidi ya wanasiasa ambao wanapandikiza
chuki, ubaguzi na fitina, kwani watu hao wanataka kubomoa misingi
mizuri ya umoja, upendo na mshikamano wa Taifa uliojengwa na waasisi wa
Taifa hili.
Rais
Magufuli alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aliyehudhuria mkutano huo, kwa hatua
mbalimbali anazozichukua kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar huku
akibainisha kuwa tatizo la maji linalovikabili visiwa vya Zanzibar
litakwisha baada ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa maji utakaofadhiliwa
na Serikali ya India kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 92, na
mradi mwingine utakaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 21.
Aidha,
Rais Magufuli alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri
vinayofanya katika kusimamia amani visiwani humo huku akivihakikishia
kuwa yeye akiwa kiongozi wao anawaunga mkono.
Pamoja
na Rais Shein Mkutano huo ulihudhuriwa na Mke wa Rais wa Kwanza wa
Zanzibar Mama Fatma Karume, Mawaziri na Viongozi wa Siasa na Dini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Unguja
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )