Mbunge
wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshauri kutazamwa
mchakato mzima wa ubinafsishaji kwa kufanya ukaguzi maalumu wa sera ili
kutoa mapendekezo ya kurekebisha makosa yaliyofanyika.
Amesema katika kufanya hivyo, suala la Airtel linaweza kushughulikiwa na kupata matunda mazuri zaidi.
Zitto
katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa Desemba 22,2017
amesema Serikali inaweza kuunda tume kutazama namna ubinafsishaji
ulivyofanyika na kuchukua hatua za kisayansi baada ya matokeo ya kazi
hiyo.
Amesema akiwa kiongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) walifanyia kazi sera ya ubinafsishaji.
“Katika
kila taarifa yetu ya mwaka tulikuwa na sehemu maalumu iliyoeleza
ufuatiliaji wetu wa utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji,” amesema.
Zitto
amesema ubinafsishaji wa iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ni
suala walilolitolea taarifa mara kadhaa bungeni na ya mwisho ilikuwa
Januari 2015.
“Ni
ukweli usio na shaka kuwa kampuni ya Celtel (sasa Airtel) haikulipa
chochote kuwezesha kumiliki hisa kwenye Celtel Tanzania na pia uuzwaji
wa Celtel kwenda Zain na kisha Airtel ulisababisha Tanzania kupoteza
mapato ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax),” amesema.
Hata hivyo, amesema kunahitajika kushughulikia suala la Airtel kwa muktadha wa kazi nzima ya ubinafsishaji nchini.
Zitto
amesema PAC iliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kufanya uchunguzi baada ya ubinafsishaji wa mashirika kadhaa,
ikiwemo Benki ya NBC na matokeo waliyawasilisha bungeni.
“Uuzwaji
wa NBC nao ulikuwa ni wa bure na huwezi kushughulika na kampuni
mojamoja bila kutazama muktadha mzima wa ubinafsishaji wa mashirika ya
umma,” amesema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )