Featured
Loading...

JWTZ Kuwa Mwenyeji Wa Mazoezi Ya Majeshi Ya Nchi Za Jumuiya Ya Afrika Mashariki Mkoani Tanga

Jeshi  la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanatarajia kuwa wenyeji wa zoezi la mafunzo yaitwayo Ushirikiano imara 2018 litakaloshirikisha nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda ambapo mafunzo yataendeshwa mkoani Tanga .

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Mkuu wa Mafunzo na Operesheni  (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga amesema kuwa, zoezi hilo ni la medani na litafanyika katika wilaya za mijini pamoja na Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Ameeleza kuwa zoezi hilo litaanza rasmi tarehe 05 mpaka 21, sambamba na hilo mafunzo hayo yatalenga kujenga uwezo wa kukabiliana na uharifu pamoja na majanga.

Pia amesema kuwa dhumuni la zoezi hilo kikanda ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji, kuimarisha mahusiano baina ya nchi, majeshi ya Afrika Mashariki pamoja na taasisi zingine za kiraia ambazo zitashiriki zoezi hilo.

Sanjari na hilo kutakuwa na kazi za kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali zikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu pamoja na vyoo katika Shule ya msingi ya Machemba iliyopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, pia kutakuwa na utoaji wa huduma za tiba kwa wananchi katika eneo la zoezi.

Hivyo, Meja Fabian ametoa rai kwa wakazi wa Tanga kuonyesha ukarimu pamoja na amani baina ya wageni watakaokua kwa kipindi chote cha mafunzo kama walivoonyesha mwaka jana ambapo mafunzo yalikua yakiendeshwa.

TTCL Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Kupunguza Wafanyakazi 550


 

Wafanyakazi Watano Wa NEMC Wafikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma Za Kughushi Saini Ya Waziri Januari Makamba

Wafanyakazi watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi, ikiwamo kula njama na kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka hayo jana Jumatano Oktoba 31, 2018 na wakili wa Serikali, Faraja Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Akisoma mashtaka hayo, Nguka alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh 160 milioni.

Wakati washtakiwa hao wakisomewa mashtaka hayo,  mshtakiwa mwenzao, ofisa mazingira wa Nemc, Magori Wambura (38) ambaye hakuwepo mahakamani, imetolewa hati ya kumkamata ili asomewe mashtaka yanayowakabili wenzake.

Washtakiwa waliosomewa mashtaka ni ofisa mazingira wa Nemc, Deusdith Katwale (38) mkazi wa Ubungo Msewe, mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi (33) mkazi wa Ubungo Msewe, sekretari wa baraza hilo, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisa Mwaruka Mwaruka (42) mkazi wa Ukonga Mombasa na ofisa mazingira NEMC, Lilian Laizer (27) mkazi wa Ukonga Mombasa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa  kati ya Septemba  27, 2016 na April Mosi, 2018 Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  Oktoba 17, 2017 Dar es Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba, 2017 Dar es Salaam kwa nia ovu walighushi saini ya Makamba katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la nne,  mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba  2017 katika ofisi za Nemc Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 cha Oktoba 17, 2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la tano, washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 27 na Aprili 6 ,2018 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh160 milioni toka kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na Nemc kitendo ambacho si kweli.

Katika shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba27, 2016 na Aprili 6, 2018 Dar es Salaam waliisababishia Nemc hasara ya Sh160 milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mashtaka ya uhujumu uchumi Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza hadi Mahakama Kuu.

Washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14, 2018.

Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali Yapewa Siku 14 Zaidi Kuwasilisha Taarifa Za Miradi Na Matumizi Ya Fedha Za Mwaka 2016 Na 2017


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa siku kumi nne zaidi (14) kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuhakikisha yanawasilisha taarifa za miradi na za fedha za mwaka 2016 na 2017 zilizokaguliwa kwa Msajili wa Mashirika hayo kabla ya kufutiwa usajili wao.

Tamko hilo limetolewa jana jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Ufafanuzi ulitolewa kuwa, “Siku ya tarehe 28 Septemba, 2018, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile alikutana na wawakilishi wa vyombo vya habari na kutoa maagizo yakuyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwasilisha taalifa zao kwa Mashirika hayo ikiwa ni pamoja na taarifa za miradi na taarifa za fedha zilizo kaguliwa kwa mwaka 2017 na 2018”, alibainisha DKT. Jingu.

Dkt Jingu amefafanua kuwa, maagizo hayo yalipaswa kutekelezwa ndani ya siku thelathini (30) kuanzia tarehe 28.9.2018 ya agizo lilipotolewa na Serikali. Hata hivyo imeelezwa kuwa mwitikio wa utekelezaji umekuwa wa kuridhisha kutokana na ukweli kuwa Mashirika mengi yamezingatia maelekezo ya Serikali.

Aidha, Wizara imepokea maombi kutoka Ofisi ya Baraza la Taifa la NGOs na baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakiomba kuongezwa muda kidogo ili waweze kukamilisha maandalizi ya taarifa zao na kuziwasilisha haraka. 

Kutokana na kutambua nafasi ya NGOs katika maendeleo ya Taifa, Serikali imeridhia kuongeza siku kumi na nne (14) kuanzia leo (31/10/2018) ili kuwapa fursa wale ambao walikuwa bado hawajatimiza maelekezo hayo kutokana na sababu mbalimbali kufanya hivyo. 

“Nasisitiza kuwa hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza kwa wale ambao hawatakuwa wamewasilisha taarifa hizo ndani ya muda wa nyongeza. Shirika ambalo litakuwa halijawasilisha taarifa Wizara itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria”. alisisitiza Dkt. Jingu.

Katibu Mkuu huyo amerudia kuhakikishia umma kuwa, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa NGOs kwa maendeleo ya nchi. Msisitizo wa Serikali wa uwazi na uwajibikaji unalenga kuwezesha Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo kutambua vizuri zaidi mchango wa NGOs  katika shughuli za maendeleo.

 Pia kama ilivyo kwenye sekta nyingine, uwazi na uwajibikaji utasaidia kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali zinazotolewa na wadau wa maendeleo kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwa kichocheo katika kufikia azma ya maendeleo jumuishi.

Akizungumza katika Mkutano huo, katibu Mkuu wa Braza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Ismail A. Suleiman ameishukuru Serikali kwa kuridhia ombi nyenyekevu la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za fedha na miradi ili  kuwezesha NGOs kutimiza takwa la  agizo hio.

Bw. Ismail amebainisha kuwa kanuni mpya za NGOs (2018) zilizotangazwa tarehe 19/10/2018 kwa kiasi kikubwa zimezingatia utekelezaji wa kanunni za maadili; hivyo Braza la NGOs litaunda kikosi kazi kuzipitia na kutoa maoni kwa lengo la kuboresha utendaji wa NGOs kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu.

Baraza la NGOs limewataka wanachama wake wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuhakikisha kuwa wanatekeleza kazi zao kwa mujibu wa katiba za mashirka yao ili kushirikiana na Serikali katika kuchochea ustawi na maendeleo ya watu hususan kunufaisha makundi yote ya kijamii.

Maagizo haya kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanakuja mwezi mmoja baada ya AGIZO LA Serikali kutolewa likizitaka NGOs zote nchini pamoja na mambo mengine kuwasilisha taarifa zao za kazi na matumizi ya fedha ya miradi wanayoitekeleza. 

Imeelezwa kuwa hadi taarifa hii inatolewa zaidi ya Mashirika 2000 yamewasilisha taarifa zao na wengi wanaendelea kuitiki maelekezo hayo.

Msafara Wa Waziri Lugola Wanusurika Kugongwa Na Basi Lililokua Mwendokasi Likiovateki Katika Kona Gairo

 
Na Felix Mwagara, MOHA-Gairo.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amenusirika kupata ajali wilayani Gairo, Mkoani Morogoro baada ya basi la Hekima za Mungu kuovateki katika kona wakati gari la waziri huyo likiwa eneo sahihi.

Tukio hilo lilitokea jana saa 6:04 mchana wakati Waziri huyo alipokua anatokea Mjini Dodoma kuelekea Jijini Dar es Salaam, katika eneo la nje kidogo ya Mji wa Gairo, basi hilo likiwa mwendokasi likiovateki katika kona, ndipo dereva wa gari la Waziri Lugola alipunguza spidi ili kuiepuka ajali hiyo.

Hata hivyo Basi hilo lilipopita, Waziri huyo aliekeza gari hilo lifuate kwa nyuma mpaka walikamate, hata hivyo Basi hilo lilikamatwa na dereva wa basi hilo kukaguliwa kama alikua na sifa ya kua dereva.

Bara baada ya kumkagua dereva huyo, Waziri Lugola alizungumza na abiria wa basi hilo lenye namba za usajili T140 AZZ ambalo lilikua linatoka Dar es Salaam kuelekea Mjini Kahama mkoani Shinyanga.

“Kwanini mnashindwa kukemea hii tabia ya huyu dereva, mnataka awaue?, alitaka kusababisha ajali mbaya sana hapa, nanyi mmekaa kimya, mnafanya makosa kutokuripoti hii tabia mbaya kabisa,” alisema Lugola.

Aliongeza kua, yeye ni Waziri ambaye anakemea mwendokasi na kiuwataka madereva nchini waendeshe kwa umakini, lakini dereva huyo anashindwa kufuata sheria za usalama barabarani, hivyo anapaswa kuchukuliwa hatua na iwe fundisho kwa madereva wenye tabia kama hiyo.

Licha ya Dereva wa Basi hilo, Isaac Vian alikiri kosa hilo na kuomba msamaha lakini Waziri Lugola aliekeza akamatwe lakini atakapofika mwisho wa safari.
 

Zitto Kabwe Kanyimwa Dhamana

Jebra Kambole, wakili wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe anayeshikiliwa na polisi kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, amesema mwanasiasa huyo amenyimwa dhamana.

“Polisi wamesema hawawezi kumuachia kwa leo wanaendelea kumshikilia kwa ajili ya mahojiano. Wamesema hawawezi kumpa dhamana,” amesema Kambole .

Zitto alikamatwa na polisi leo saa 5 asubuhi na kupelekwa kituo cha polisi Oysterbay ambako alihojiwa kwa takribani saa tatu, kisha kuhamishiwa kituo kikuu cha polisi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas  leo amewaeleza wanahabari kuwa wanamshikilia Zitto kutokana na matamshi aliyoyatoa hivi karibuni.

Jana, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018 kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno amesema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

Katika ufafanuzi wake leo, Kambole amesema Zitto alipofikishwa Oysterbay aliandika maelezo, kuhojiwa akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.

“Baada ya kuhojiwa aliandika maelezo ya awali na aliwaeleza kuwa kama kuna maelezo mengine atayatoa mahakamani,” amesema Kambole.

“Hakuna chochote kilichoendelea na sheria inamruhusu kama unaona hulazimiki kutoa maelezo. Maelezo kuhusu makosa yake hajayatoa na hakulazimishwa kuyatoa anasubiri kama akipelekwa mahakamani atayatoa huko.”

Ameongeza, “Wamesema dhamana yake wameishikilia na kosa lake ni kutoa maneno ya kichochezi.”

Waliopoteza Ajira Kupata Mafao Yao Mwezi Ujao


Mamlaka  ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imesema mifuko ya PSSSF na NSSF iko katika hatua za mwisho za kujenga mifumo ya ndani ya ulipaji wa fao la upotevu wa ajira, maarufu Fao la Kujitoa.

Vilevile, imesema Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), utaanza kupokea maombi ya fao la upotevu wa ajira kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu (Alhamisi), likiwalenga waliopoteza ajira baada ya sheria kuanza kazi Agosti Mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, kutakuwa na mifuko miwili nchini ambayo ni PSSSF inayohudumiwa watumishi wa umma ambayo ni muunganiko wa mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF.

Pia kuna mfuko wa NSSF ambao unahudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Hayo yalisema jana na Meneja Mawasiliano wa SSRA, Sara Kibonde, alipozungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua kama mifuko hiyo imeshaanza kutoa fao la upotevu wa ajira ambalo limetajwa katika sheria mpya ya mfuko wa hifadhi ya jamii.

"Kukosekana kwa utaratibu wa kinga ya kipato kwa wafanyakazi wanaopotea ajira kumesababisha wafanyakazi kujitoa uanachama na kuchukua michango yao, ili kujikimu baada ya kupoteza ajira kiasi cha kupewa jina la fao la kujitoa na hiyo ilitokana na kukosekana kwa mbadala wake," alisema.

Kwa mujibu wa Kibonde, ukuaji wa sekta binafsi umechangia kuwa na mabadiliko katika soko la ajira na kuchangia ongezeko la fursa za ajira zenye masharti ya muda mfupi ya ajira na kusababisha wafanyakazi kuomba kujitoa uanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii mara mikataba yao ya ajira inapokoma.

Alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha wafanyakazi walio kwenye kundi la masharti ya ajira za kudumu ndiyo lina matukio mengi ya wanachama kujitoa.

"Kuwapo kwa idadi kubwa ya wafanyakazi wanaojitoa kutoka kwenye kundi la wafanyakazi wenye mikataba ya ajira ya muda mrefu kunaashiria kwamba baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakijitoa bila sababu za msingi."

Alisema mwanachama anayechukua michango yake anakuwa amepoteza sifa ya kulipwa mafao ya pensheni atakapotimiza umri wa kustaafu na ndiyo maana sheria mpya imeleta utaratibu mbadala ambao utakuwa kinga ya kipato.

Kwa mujibu wa kanuni za sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii ya mwaka 2018, utaratibu wa kujitoa kwenye mifuko hiyo umeainishwa kuwa mafao ya kujitoa yatakuwa asilimia 33.3 ya mshahara wa mwezi wa mwanachama husika.

Pia, muda wa ulipaji mafao ni miezi sita na mwanachama atalipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 18 na mwanachama aliyechangia chini ya miezi 18 atalipwa asilimia 50 ya michango yake.

Kanuni hizo pia zinabainisha kuwa kama mwanachama atakuwa hajapata ajira baada ya miezi 18, atamwandikia Mkurugenzi Mkuu wa mfuko kuomba kuhamishia michango yake kwenye mfuko wa hiari na kuendelea kuchangia.

Vigogo waliojilimbikizia mashamba makubwa ya mkonge Kuanza Kuchunguzwa


Vigogo waliojilimbikizia mashamba makubwa ya mkonge wako hatarini kupokwa kutokana na mpango wa serikali kuyafanyia ukaguzi wa kuwabaini walioyatelekeza bila kuyaendeleza.

Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisema serikali itaanza kufanya ukaguzi mashamba yote ya mkonge nchini kwa lengo la kubaini yale ambayo hayafanyi vizuri ili wayafute na kupatiwa watu wengine watakaokuwa na uwezo wa kuyaendeleza.

Aidha, Lukuvi ameijia juu Bodi ya Mkonge Tanzania kwa kushindwa kusimamia vizuri kampuni zinazozalizasha zao hilo ambapo mengi yao uendeshaji wake hauna tija kwa kuwa hayatoi ajira za kutosha kwa wananchi wanaozunguka eneo husika sambamba na kuikosesha serikali mapato.

Lukuvi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na uongozi wa kampuni ya kuzalisha mkonge ya LM Investments Ltd iliyopo katika kijiji cha Ndungu Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro wakati akikamilisha ziara yake ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Hai, Moshi na Same.

“Mashamba mengi ya mkonge hapa nchini uendelezaji wake hauna tija, hauridhishi na wamiliki wake wanahodhi tu maeneo jambo linaloikosesha serikali mapato, huku wengine wakitumia mashamba hayo kukopea fedha katika benki,” alisema Lukuvi.

Alisema pamoja na kuwapo Bodi ya Mkonge ambayo ina jukumu la kusimamia uendeshaji zao hilo, lakini imeshindwa kufanya kazi ipasavyo, hivyo kusababisha makapuni ya kuzalisha mkonge kufanya yanavyotaka.

“Kama bodi ya Mkonge wameshindwa kuchukua hatua kwa wale wasiofanya vizuri katika uzalishaji wa mkonge, basi sisi kama Wizara ya Ardhi tutafanya ukaguzi kwa mashamba yote ya mkonge ili tubaini wale wasiofanya vizuri na tuwanyang’anye na tuwapatie watu wengine wenye uwezo,” alisema Lukuvi.

Kauli ya Lukuvi inafuatia kutoridhishwa na uendeshaji wa Shamba la Mkonge la Ndungu lenye ukubwa wa hekta 1,230 linalomilikiwa na Kampuni ya LM Investments Ltd. 
Shamba hilo limekuwa na mgogoro na wananchi wa vijiji vitatu vya Ndungu, Gonja Mperani na Msufini. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya LM Investments Ltd, Allan Chellangwa, shamba hilo limekuwa likizalisha wastani wa tani 30 mpaka 50 kwa mwezi na lengo ni kuzalisha tani 50 kwa mwezi huku wafanyakazi 24 wakiwa wameajiriwa.

Maelezo hayo yalimshtua Lukuvi ambaye alisema uwiano wa hekta 1,230 na ajira za watu 24 hauendani na kueleza kuwa lengo la serikali kutoa mashamba makubwa kwa wawekezaji ni kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kupata mapato kupitia kodi na kusisitiza serikali haiwezi kuacha shamba lenye ukubwa huo kutoa ajira za watu wachache tu.

Wenyeviti wa vijiji vya Msufini, Gonja Mperani na Ndungu waliiomba serikali kuwapatia ekari 100 kila kijiji ili ziwasaidie katika shughuli zao. Mwenyekiti wa Kijiji cha Msufini, Omar Mganga, alimueleza Lukuvi kuwa kijiji chake kimekuwa na uhaba wa ardhi jambo linalosababisha wananchi wa eneo hilo kukosa maeneo ya makazi na ya kuzikia.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vyote vitatu, Lukuvi aliwaeleza kuwa moja ya kazi ya serikali ni kuondoa kero, kulinda wawekezaji na kutetea wanyonge na kufafanua kuwa jukumu la serikali siyo kufukuza wawekezaji, ila ni kutaka kuwa na wawekezaji wenye tija, watakaoleta teknolojia mpya pamoja na kuongeza pato la taifa.

Katika kutatua mgogoro huo, Lukuvi aliamuru vijiji hivyo vitatu vipatiwe jumla ya hekta 300 kutoka hekta zinazomilikiwa LM Investments Ltd 1,230 ambapo hekta 71 ni zile zilizoongezwa tofauti na makubaliano ya umilikishwaji mwaka 1998 na nyingine zitatoka ndani hekta zinazomilikiwa na kampuni ambapo kila kijiji sasa kitapatiwa hekta 100 jambo lililopokelewa kwa furaha na wananchi wa vijiji hivyo.

Kangi Lugola Atoa Maagizo Mazito Baada Ya Kubaini Makanda wa Polisi Hawatekelezi Maagizo Yake Anayotoa


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka makamanda wa polisi wa mikoa kujitathmini kama wanatosha katika nafasi hizo, vinginevyo wajiandae kuziachia.

Lugola alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo kikuu cha polisi jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema baadhi ya makamanda hawajaanza kutekeleza maagizo yake kwa madai kuwa yamekuwa yakitolewa kisiasa zaidi.

“Wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) wawe mguu sawa, maana hawajui siku wala saa nitakapoibuka kwenye vituo na mikoa yao ili kuangalia maagizo yangu kama yanatekelezwa au la, wengi wataondoka na kuwapisha wenye weledi na uwezo wa kufanya kazi,” alisema Lugola.

Alisema atamuandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuhusiana na maagizo anayoyatoa kwamba lazima yatekelezwe na makamanda wa mikoa, lakini atakayeshindwa atalazimika kuwapisha wenzake.

Waziri Lugola alirudia kauli yake kuhusu makosa yenye dhamana kwamba lazima watu wapewe dhamana iwe sikukuu, usiku au siku za mwishoni mwa wiki na kuwa Mtanzania yeyote ana haki ya kumwekea dhamana mtuhumiwa.

“Inspekta Jenerali wa Polisi namuelekeza kwamba kila raia wa nchi hii awe mfugaji, mvuvi, mkulima au mfanyabiashara anayo haki ya kumdhamini Mtanzania mwenzake,” alisema.

Lugola alisema, “Kinachotakiwa ni kutimiza vigezo vya huyo anayemdhamini kama anafahamika, anatambulika na ataweza kumleta huyo aliyemdhamini kwenye kituo cha polisi siku ambayo ameelekezwa kwenye hati yake ya dhamana.”

Akizungumza katika ziara hiyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto aliahidi kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza ikiwemo ya kutotolewa dhamana kwa watu wanaostahili, kukosekana kwa taarifa za watuhumiwa na kukosekana kwa kibali cha kuhalalisha kuuzwa kwa pikipiki zilizokamatwa na kukosekana wamiliki wake.

Makamu wa Rais agoma kufungua stendi ya mabasi Kibaha


Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekataa kuzindua stendi kuu mpya ya Mailmoja Kibaha mkoani Pwani, akiwa katika ziara yake mkoani humo.

Hatua hiyo ameifikia kutokana na kupata wasiwasi wa utekelezaji wa mradi kuwa na baadhi ya mapungufu ambapo amedai baada ya kufanya uchunguzi wiki mbili ama tatu zijazo atakwenda kuuzindua. 
 
Akizungumza katika stand hiyo, Samia alieleza, kuna minong’ono wameisikia kuhusu mradi huo hivyo ni jukumu lake kuibeba na atakapo jiridhisha atarudi kwa mara nyingine  .
 
Hata hivyo, alisema atakutana na mkuu wa wilaya, mkurugenzi na mkuu wa mkoa kuzungumzia suala hilo. 
 
“Msishtuke kwa hili ni kawaida kwa kuchukua hatua za aina hii ili kujiridhisha kwa maslahi ya halmashauri, mkoa na watumiaji kijumla “
 
“Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni sikivu na kusikia malalamiko ya wananchi, tumepata malalamiko kidogo kuhusu stand hii, serikali ni ya uwazi na ukweli hivyo sitofungua stendi “alisisitiza Samia. 
 
Samia alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Jennifer Omolo na mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama na wahusika waliohusika kufanikisha mradi huo.
 
Nae waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa -TAMISEMI ,Selemani Jafo alisema yeye kama waziri wapo wataalamu wanaohakiki lakini ameridhishwa na kazi hiyo .
 
“Kwani kila kazi ina changamoto za kibinadamu, hasi na chanya, lakini wamejitahidi  “alisema Jafo.

Jafo alieleza, mradi huo umepata msaada wa mkopo nafuu kutoka bank ya Dunia ambao wamepata fedha za kimarekani dollar milioni 255 .

Alielezea , wanagusa miji 18 na wanachokifanya wanagusa stendi tisa, barabara za miji kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa ya kisasa. 
 
Wakitoa kero ya stand hiyo, madereva pikipiki walidai eneo lililotengwa kwa ajili yao halina sehemu ya kujikinga hivyo kusababisha usumbufu wakati wa mvua na jua. 
 
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Jennifer Omolo alisema katika stendi ndogo ya awali walikuwa wakikusanya ushuru sh. 950.000  kwa siku ambapo sasa wanakusanya sh. milioni 1.6 .
 
Alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 2.9 na walishamlipa mkandarasi bilioni 2.7 ,stendi hiyo itakuwa na mabanda kumi ya kukatia tiketi, mawakala 40 ,eneo la tax, na wafanyabiashara ndogondogo wanaojiingizia kipato kwa kuuza biashara zao wapo 100 .
 
Samia akiwa katika ziara yake Kibaha vijijini na mjini pia alipata fursa ya kutembelea mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge kujionea namna unavyoendelea.

Diamond na Rayvanny wafunga mitaa Posta Dar es Salaam


Wasanii kutokea WCB, Rayvanny na Diamond Platnumz  jana Jumapili October 28, walifunga baadhi ya mitaa Posta Dar es Salaam kutokana na utengenezaji wa video ya wimbo wao mpya.

Tukio hilo lilivuta umati mkubwa wa watu licha ya jana kutokuwa ni siku ya kazi kitu kilichopelekea baadhi ya shughuli kusimama kwa muda.

Bila shaka wimbo huo utakuwa wa tatu kwa Diamond Platnumz kumshirikisha Rayvanny baada ya nyimbo kama Salome na Iyena.

Rais Dkt. Magufuli Akutana Na Kuzungumza Na Wanunuzi Wa Korosho Jijini Dar Es Salaam Na Kutoa Msimamo Wa Serikali Kuhusu Bei Ya Korosho


Rais John Magufuli ametoa msimamo wa Serikali kuwa bei ya korosho isipungue Sh3000 kwa kilo moja.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 28, 2018 alipokutana na wadau na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


Hayo yamejiri baada ya wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuingia kwenye mgomo wa kuuza zao hilo la Korosho kwa kile walichokidai kushuka kwa bei ya zao hilo ukilinganisha na miaka miwili iliyopita huku gharama za uzalishaji zikiwa zimepanda.

Kufuatia mgomo wa minada ya siku mbili, Oktoba 26, Rais Magufuli, alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwaeleza kuwa anaunga mkono hatua ya maamuzi hayo ya wakulima na kusema yuko nao bega kwa bega.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba na watendaji wengine wa serikali.


"Nawataka wafanyabiashara muelewe kuwa, hakuna korosho itakayouzwa chini ya shilingi 3,000. Kama hamtanunua, mniambie.

"Serikali tunaunga mkono wakulima kukataa bei za korosho. Ndio maana kiongozi wa Bodi ya Korosho alipowatisha wakulima kuwa lazima wakubali, tumemuondoa, na hatorudi huko."Amesema Rais Magufuli


Baba Mzazi wa Mo Dewji Afunguka Alivyompata Mwanaye....Amshukuru Rais Magufuli

Familia ya bilionea Mohammed Dewji, imesimulia namna kijana wao alivyoachiwa na watekaji usiku wa kuamkia leo.

Baba yake mzazi Gullam Dewji Hussein ameviambia vyombo vya habari kuw alipigiwa simu leo alfajiri Oktoba 20, 2018 akielezwa kuwa mwanae amepatikana.

Gullam amesema alijulishwa kuwa mwanaye amepatikana akiwa katika gari ambalo lilitelekezwa katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa.

Amesema Mo Dewji baada ya kushushwa katika gari hilo alitembea kutafuta msaada wa simu.

Amebainisha kuwa baada ya kupokea simu hiyo alifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumuona mwanaye.

“Namshukuru Mungu nimemkuta Mo akiwa salama na haraka nilimpeleka nyumbani lakini tumemkuta ana majeraha kidogo ila jambo la kushukuru ni kwamba yuko hai,” amesema Gullam.

“Tulipofika nyumbani tulianza kufanya mawasiliano na Jeshi la Polisi kwa kuwapa taarifa kuwa kijana wangu nimempata na wao (polisi) walifika nyumbani kwangu Oysterbay.”

Gullam amemshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha kupatikana kwa mwanaye.

Mo alitekwa saa 11 alfajiri ya Oktoba 11 mwaka huu, katika hotel ya Colosseum iliyoko Oysterbay jijini Dar es Salaam, alipokwenda kufanya mazoezi.

Waziri Mkuu Amkabidhi Waziri Jafo Orodha Ya Watumishi.....Ni wa halmashauri ya wilaya ya Bahi waliogoma kuhamia kituo cha kazi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI, Selemani Jafo orodha ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ili awachukulie hatua baada ya kugoma kuhamia katika kituo chao cha kazi na kuendelea kuishi jijini Dodoma.

Amemkabidhi orodha hiyo jana (Ijumaa, Oktoba 19, 2018) baada ya mkuu wa wilaya hiyo Bibi Mwanahamisi Mukunda kusoma taarifa ya wilaya, ambayo pamoja na mambo mengine alieleza kuwa watumishi wote wameshamia kwenye kituo chao cha kazi na wanaishi. Waziri Mkuu alikuwa katika kikao na Watumishi wa Halmashuri hiyo.

“Mkuu wa wilaya umedanganywa watumishi bado wanaishi jijini Dodoma, walichokifanya baadhi wamejiunga watatu na wamekodi chumba kimoja. Namkabidhi Waziri wa TAMISEMI orodha ya watumishi hawa ambao wamegoma kuishi kwenye kituo chao cha kazi ili uwashughulikie”

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wamegoma kuhamia katika kituo chao cha kazi licha ya Serikali kuwataka kufanya hivyo.”Maelekezo hatuyatoi kwa ajili ya kujifurahisha, bali tunataka utekelezaji ufanyike ili wananchi waweze kuhudumiwa ipasavyo.”

Jumatano, Juni 27, mwaka huu, Waziri Mkuu wakati akizinduavituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, aliwaagiza watumishi wa Halmashauri hiyo wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wahamie kituoni kwao.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi. “Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini Dodoma wawe wamehamia hapa ifikapo Julai 30 mwaka huu na wasiohamia nipewe majina yao.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Bahi wakiwemo madiwani na wakuu wa idara wahakikishe wanamaliza tofauti zao na washirikiane katika kufanyakazi kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Mpalanga yenye uwezo wa kukaliwa na walimu sita, ambapo amesema ameridhishwa na ujenzi huo. Mradi huo unagharimu zaidi ya sh. milioni 140.

Pia Waziri Mkuu amezindua daraja la Chipanga ambalo ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 2.18 na kisha alitembelea kituo cha Afya cha Bahi ambako alikagua wodi ya wazazi na kuzungumza na akinamama ambao waliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya.

Muonekano wa Gari Lililomteka Mo Dewji Baada ya Kutelekezwa Leo Asubuhi

Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama leo asubuhi Oktoba 20, 2018 wameonekana wakikagua na kuchukua vielelezo katika gari inayodaiwa kutumika kumteka mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’.

Gari hiyo aina ya Toyota Surf yenye namba T314AXX  imetelekezwa katika barabara ya Ohio karibu na lango kuu la kuingilia  viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa chache baada ya mfanyabiashara huyo kutupwa na watekaji katika viwanja hivyo.

Kufuatia kuonekana kwa gari hilo, barabara hiyo imefungwa.

Jana, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alizungumza na waandishi wa habari na kuonyesha picha ya gari hilo, akieleza kuwa lilitumiwa na watekaji.

Hata hivyo, jana katika picha hizo gari hilo lilikuwa na namba AGX 404 MC.

Magari saba ya polisi yameegeshwa kando ya barabara hiyo huku askari wakiendelea na uchunguzi.

Breaking News: Msikilize Hapa Mo Dewji Akiongea Baada ya Kupatikana Leo Usiku

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' alitupwa kwenye Viwanja vya Gymkhana katikati ya jijini la Dar es Salaam.

Akizungumza leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 Mambosasa amesema polisi walipata taarifa leo saa nane usiku kuwa mfanyabiashara huyo amepatikana na watekaji walimchukua kwenye gari waliyotumia kumteka na kumtupa katika viwanja hivyo.

“Polisi tulipata taarifa kwamba amepatikana, watekaji walimchukua kwenye gari ile ile waliyotumia kumteka na kwenda kumtupa katika viwanja hivyo,” amesema Mambosasa.

“Tangu alivyotekwa pale hoteli ya Collesium (alfajiri ya Oktoba 11, 2018) gari ya watekaji iliondoka kasi na baada ya dakika  15 Dewji alijikuta amewekwa kwenye chumba akiwa amefunikwa  ili asiwatambue watekaji.”

Amebainisha kuwa mfanyabiashara huyo amewaeleza kuwa watu waliomteka walikuwa wakizungumza moja ya lugha za Afrika Kusini.

“Baada ya kumhoji ameeleza kuwa alitambua lugha walizokuwa wakizungumza kwamba ni kama za Afrika Kusini. Mashaka yetu kuwa waliofanya tukio hili sio Watanzania yamethibitishwa na Dewji mwenyewe,” amesisitiza.

 
“Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.” — Amesema Mohammed Dewji

BREAKING NEWS: Mo Dewji Kapatikana Akiwa Mzima

Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni ya METL, Mohammed Dewji (MoDewji) amepatikana na kurudi nyumbani kwake salama, saa 9 na dakika 15 Alfajiri hii ya October 20.

Mzee Gulam Hussein amethibitisha mwanaye kupatikana na kurudi nyumbani salama

Pia 'personal Assistant ' (PA) wa Mohammed Dewji Barbara Gonzale amethibitishia  kuwa Mo amepatikana na kuzungumza maneno yafuatayo;

“Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.” — Mohammed Dewji

Destination Uncharted: Hidden Animal Wars - YouTube


big animals war


Animal War - Snake vs Crocodile - Lion vs Tiger


© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top